Siku moja baada ya siku yake ya kuzaliwa mwezi Mei, Olalekan Jacob Ponle aliweka picha katika mtandao wa Instagram akiwa amesimama pembeni ya gari lake la kifahari aina ya Lamborghini huko Dubai.
"Acha kuwaruhusu watu wakufanye ujisikie vibaya kutokana na jinsi ulivyopata utajiri wako''
Katika picha hiyo ameonekana amevaa mavazi ya kifahari. Kuanzia juu hadi miguuni amevalia mavazi ya Gucci.
Mwezi mmoja baadae Mnaijeria kwa jina ''mrwoodbery" anavyojiita kwenye mtandao wa Instagram, alikamatwa na polisi wa Dubai kwa kosa la utakatishaji fedha na uhalifu wa mtandao.
Mnaijeria mwingine maarufu kukamatwa ni Ramon Olorunwa Abbas, "hushpuppi" au ''Hush'' kama anavyojulikana na wafuasi wake zaidi ya milioni mbili kwenye mtandao wa Instagram.
Polisi wa Emirate wamesema kuwa wamepata kiasi cha dola milioni 40, magari 13 ya kifahari yenye thamani ya dola milioni 6.8, kompyuta 21,simu 47 na anuani za watu karibu milioni mbili waliowasiliana nao.
Bwana Abbas na Bwana Ponle walirudishwa mara moja nchini Marekani ambako walishtakiwa katika mahakama ya Chicago kwa mashtaka ya wizi wa mamilioni ya dola kwa njia ya uhalifu wa kimtandao .
Wote hawajaitwa kukiri au kukubali mashtaka wanayoshtakiwa, na hadi sasa hawajapatikana na hatia.
Glen Donath aliyekua mwendesha mashtaka zamani mjini Washington anasema wanaume hawa "walizidi kujidai kwani walijinadi kupita kiasi katika mitandao ya kijamii ".
Taarifa hii iliwashangaza wengi ambao wamekua wakifuatilia maisha yao ya hali ya juu kwenye mitandao ya kijamii, wakijiuliza wanaume hawa wanatoa wapi pesa kiasi hicho.
Bila kujua walichokua wakikifanya, kwa kuonesha maisha yao ya hali ya juu katika mitandao wa Instagram na Snapchat, wanaume hawa walikua wakitoa utambulisho wao kwa majasusi wa Marekani.
Kwa sasa, wanashtakiwa kwa kudanganya kuwa ni wafanyakazi wa kampuni mbalimbali nchini Marekani , kuandika barua pepe wakiwadanganya watu ambao waliwatumia mamilioni ya dola kwenye akaunti zao.
Katika mtandao wa Instagram , "hushpuppi" anajitambulisha kama mtaalamu wa ujenzi, na hata kuna picha zinazoonesha nyumba anayoijenga. Lakini ''nyumba'' hizo alizitumia kama njia ya ulaghai na wizi, kulingana na wapelelezi.
"Mfumo wetu wa maadili yetu ya Nigeria inapaswa kuangaliwa, hususan thamani tunayoipatia mali, kwa vyovyote vile unavyoipata . Ebuka Emebinah,mtaalamu wa masuala ya uchumi ." ameiambia BBC .
''Ni utamaduni ambapo watu wanaamini kwamba matokeo yanakuelezea . Hatuweki msisitizo katika mchakato na hili limejengwa kwa muda''
Walilenga timu ya ligi ya Primia.
Mwezi Aprili , "hushpuppi" alibadilisha upya makubaliano ya kukodi nyumba ya kifahari sana Dubai kwa majina yake halisi na simu yake binafsi.
Wiki mbili kabla ya kutiwa nguvuni, aliweka picha yake kwenye Instagram akiwa karibu na magari yake mawili ya Rolls-Royce akaandika ujumbe:
"Asante Mungu, kwa Baraka nyingi maishani mwangu. Endelea kuwaaibisha wale wanaosubiri niaibike''
"Maisha ya kifahari ya Abbas yanatokana na uhalifu, pia ni mmoja wa watu wanaoongoza kwa wizi wa mtandao kwa kuvamia kompyuta za watu, wizi wa pesa kwa njia ya ulaghai wakiwalenga watu kote duniani katika mfumo uliotengenezwa kwa lengo la kuwaibia mamilioni ya dola ". Ilisema taarifa ya Shirika la upelelezi la Marekani FBI kuhusu uchunguzi.
Katika kisa kimoja, kampuni ya fedha inasema iliibiwa dola $14.7 kwa njia ya mtandao, inasema kuwa fedha hizo zilikwenda kwenye akaunti za "hushpuppi" zilizpo katika nchi mbali mbali duniani.
Waraka wa mashtaka unaonyesha kuwa mtu huyo anakabiliwa na shitaka la la kuiba dola milioni $124 kutoka kwa moja ya timu ambayo haikutajwa ya Primia Ligi.
FBI limesema kuwa lilipata taarifa katika mitndao Google, Apple iCloud, Instagram na Snapchat, akaunti za benki , stakabadhi zake za usafiri, mawasiliano na washirika wake katika wizi na rekodi za utumaji wake wa pesa.
'Yahoo boys'
Takriban 90% ya barua pepe za utapeli hutoka Afrika ya magharibi kulingana na taasisi ya Marekani ya usalama wa kimtandao , Agari.
Crane Hassold anayeshughulikia uhalifu wa aina hii katika taasisi Agari. Anasema: ''Wanaofanya utapeli huu huanza kwa kuchunguza barua pepe za mawasiliano halisi katika kampuni fulani zinazofanya biasharana kuchukua anwani za barua pepe zao na baadae kupotosha mawasiliano hayo kwa kusema kuwa walibadili akaunti za benki za malipo na kuwaomba waanze kutumia akaunti hizo mpya kwa malipo''.
Bwana Ponle ambaye anatumia jina la "mrwoodberry" katika mitandao ya kijamii, alitumia jina la Mark Kain katika barua pepe'' ilisema FBI.
Anashutumiwa kuilaghai kampuni ya mjini Chicago iliyomtumia dola milioni $15.2.
Na kampuni nyingine za Iowa, Kansas, Michigan, New York na California pia zinasema kuwa ziliathiriwa na utapeli huo.
Pesa hizo baadae zilipotea kwani baada ya kutumwa kwa pesa hizo zilibadilishwa kuwa pesa mbadala zinazotumiwa kwa njia ya mtandao zinazofahamika kama 'cryptocurrency bitcoin'.
Wizi wa aina hii unaofanyika kwa njia ya barua pepe umeshamiri sana duniani na kwa kiwango kikubwa unahusishwa na Nigeria na kwamba nyota wa wizi huo Nigeria wanaitwa 'Yahoo boys'.
FBI inawatahadharisha watu wawe makini wanapofanya mawasiliano ya barua pepe zinazowahakikishia kuwa watapata pesa nyingi au wale wanaowaambia wabadili njia yao ya kawalida ya malipo.
Mwandishi wa BBC aliandikiwa hivi karibuni ujumbe ambao ulikua karibu sawa na ule unaoelezewa katika taarifa hii.
Jinsi wizi unaofahamika kama 419 na mapenzi unavyofanya kazi Mtandao wa wizi
Chanzo cha picha, Getty Images
•Mtu hukuandikia baruapepe, akikuambia kuwa anataka umsaidie kutuma pesa
•Atakwambia kuwa matatizo ya kisiasa au matatizo ya majanga mengine vinamzuwia kutuma pesa
•Atakuomba umpe akaunti yako ili atume pesa
•Hii humsaidia kuifikia akaunti yako na kuweza kuondoa pesa
•Jihadhari sana nay ale unayoyaandika katika mitandao ya kijamii kwani taarifa hizo huwasaidia kukufahamu vyema na kukukulenga.
Wakili Moe Adele, mwenye makao yake mjini Washington, anasema inasikitisha kwamba serikali ya Nigeria haijali matatizo ya vijana Wanigeria wanaojiingiza katika vitendo vya aina hii.
"Wanaviona vitendo hivi kama njia rahisi kuwasaidia katika nchi inayowapatia fursa chache na wakati mwingine haipo."
Ayo Bankole -muasisi mwenza wa Bootcamp yenye makao yake nchini Nigeria anasema: ''Kuna Wanigeria wengi wanaofanya mambo mengi mazuri duniani, lakini wanaofanya mabaya huchafua sura ya nchi.
"Kampuni nyingi siku hizi hazitumi bidhaa nchini Nigeria, kampuni nyingi hazikubali malipo kutoka imetuharibia sura ."
Katika ripoti ya mwaka 2019 kuhusu uhalifu wa kimtandao , FBI ilisema kuwa ilipokea malalamiko karibu 460,000 ya visa vinavyoshukiwa kuwa ni wizi wa kumtandao, huku zikibiwa dola bilioni $3.5 na zaidi ya dola $300 ziliweza kurejeshwa.
Hatahivyo, wengi miongoni mwa wahusika wa wizi huu hawakamatwi, na ni wachache wanofika jela kwani wizi huu huvuka mipaka na hutekelezwa kwa njia ngumu, kulingana na Glen Donath
Iwapo watapatikana na hatia Ibyaha, Bwana Abbas na Bwana Ponle wanaweza kufungwa kifungo cha miaka 20 jela.