Wanahabari wa vyombo vya habari vya humu nchini na kimataifa wameshambuliwa na genge la watu wenye visu huko Kibra siku ya Jumatatu walipokuwa wakiangazia maandamano ya kupinga serikali ya kila wiki mara mbili.
Wengine kadhaa walijeruhiwa baada ya genge la watu wenye ghasia kurushia magari yao mawe ndani ya eneo la DO la Kibra.
Kulingana na Citizen Digital, Jase Ndungu, mwandishi wa habari anayeangazia maandamano ya Kibra, genge lililojihami liliwavamia wanahabari waliokuwa wakifuatilia maandamano hayo, na kuwalazimisha kukimbia kuokoa maisha yao.
"Genge hilo lilijifanya kuwa sehemu ya waandamanaji lakini ikawa kweli walikuwa na silaha," Ndung'u aliambia Citizen Digital.
Wanahabari wamelazimika kutoroka genge la watu wenye visu kwenye gari la runinga ya Citizen huko Kibra, Nairobi.
Baadhi ya waandishi wamepoteza simu zao, pochi na vitu vingine vya thamani.
Wakati huohuo, polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi kutawanya maandamano ya kuipinga serikali Jumatatu kuhusu gharama ya juu ya maisha, baada ya upinzani kuapa maandamano yataendelea licha ya marufuku ya polisi.
Usalama ulikuwa umeimarishwa, huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwa katika maeneo ya kimkakati jijini Nairobi na kushika doria mitaani, maduka mengi yakiwa yamefungwa na huduma za treni kutoka viunga vya mji mkuu hadi wilaya kuu ya biashara zilisitishwa.
Kinara wa upinzani Raila Odinga amewataka watu kujitokeza barabarani kila Jumatatu na Alhamisi, hata baada ya maandamano ya wiki jana na vurugu na kulemeza shughuli katika baadhi ya sehemu za mji wa Nairobi.