Uchunguzi umeanza kuhusu tukio ambapo baadhi ya wanafunzi wa shule ya upili ya God-Bura eneo bunge la Suba Kusini wanasemekana kumvamia na kumjeruhi Mkuu wa shule yao.
Maafisa wa Wizara ya Elimu wanaangazia suala hilo baada ya kubainika kuwa mwalimu mkuu Collins Omondi alipokea mateke na vipigo kutoka kwa wanafunzi waliokuwa na hasira kwa madai ya kuisimamia shule hiyo vibaya.
Inasemekana wanafunzi hao walikwenda na kuvunja nyumba ya mwalimu mkuu siku ya Ijumaa asubuhi kabla ya kumshambulia kwa kuruhusu wapishi kuwapa uji bila sukari,Walihusisha utoaji wa uji usio na sukari na usimamizi mbovu wa taasisi hiyo.
Mkuu wa shule alipata majeraha kichwani na sehemu zingine za mwili. Kulingana na ripoti za polisi, wanafunzi wengi katika kidato cha 4 waliungana na wengine wa kidato cha chini kumshambulia mwalimu wao.
“Walimuamuru Omondi kuandamana nao hadi kituo cha polisi cha Magunga ili kurekodi taarifa. Wanafunzi walitaka mwalimu aeleze jinsi pesa za shule zinavyotumika," ripoti hiyo ilisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari za Suba Kusini, Paul Mbara alilaani shambulizi hilo akisema sheria hairuhusu wanafunzi na wazazi kuwashambulia walimu shuleni.
Alisema mwalimu huyo pia alipata majeraha kifuani, Omondi alikimbizwa katika hospitali ya Magunga level IV kwa uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kuelekezwa katika kituo kingine kwa ajili ya kufanyiwa X-ray. “Kushambulia walimu sio suluhu la matatizo yanayokumba shule .
Kunapaswa kuwa na njia mbadala za kutatua migogoro," Mbara alisema. Alieleza wasiwasi wake kuwa huenda suala hilo likazidi kuwa matatizo mengine yanayoweza kusababisha ufaulu wa wanafunzi.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Homa Bay Samson Kinne alisema wanachunguza suala hilo pamoja na Wizara ya Elimu. “Tungependa kuwafahamu walio nyuma ya vitendo vya wanafunzi.
Baadhi ya wazazi wanaripotiwa kuhusika na suala hilo na walionekana wakiwasaidia wanafunzi kumshambulia mwalimu,” Kinne alisema.