Zaidi ya watoto 30 wa shule wamelazwa hospitalini baada ya kuvuta gesi ya kutoa machozi iliyorushwa na polisi wa kupambana na ghasia wakati wa mazoezi ya asubuhi katika Jimbo la Osun, kusini-magharibi mwa Nigeria, vyombo vya habari nchini Nigeria vinaripoti.
Mazoezi hayo yalikuwa yakifanyika katika shule ya karibu Fakunle Comprehensive School, katika jiji la Osogbo, lakini gesi hiyo ilifika hadi kwenye chuo hicho.
Wanafunzi hao wa shule ya sekondari (upili) waliripotiwa kukimbizwa katika hospitali mbili tofauti kwa matibabu ya haraka baada ya kupoteza fahamu.
Tukio hilo lilizua hofu huku baadhi ya wazazi wakiwachukua watoto wao haraka baada ya uongozi wa shule kushauriwa kufunga siku hiyo.
Msemaji wa polisi wa Osun Yemisi Opalola aliomba radhi kwa tukio hilo na kusema maafisa hao watafanya "marekebisho ya lazima" ili kuzuia hilo kutokea tena.