Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi milioni 2.3 wameanza masomo Libya

LIBYA LIBYA MASOMO Wanafunzi milioni 2.3 wameanza masomo Libya

Tue, 5 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya (GNU) imetangaza kuwa, zaidi ya wanafunzi wapya milioni 2.3 kote Libya wameanza mwaka mpya wa masomo mashuleni wiki hii.

Taarifa ya serikali hiyo ya GNU imesema kwamba, takriban skuli 6,000 zimefungua milango yake kwa ajili ya kupokea wanafunzi wapya na wa zamani katika mwaka mpya wa masomo kwenye kona mbalimbali za Libya.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Serikali ya GNU inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdul-Hamed Dbeibah imesaidia kuandaa madarasa mapya 2,000 kwa ajili ya kupokea zaidi ya wanafunzi 45,000 katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema, serikali ya Libya imepanga kujenga shule 1,500 zaidi, ili iweze kutengeneza nafasi mpya za ajira kwa ajili ya zaidi ya wafanyakazi 10,000 wapya.

Juzi Jumapili, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilionyesha nia ya kusaidia katika juhudi za kuwekwa misingi imara ya kupatikana elimu bora nchini Libya.

Taarifa hiyo ya UNICEF imesema: "Lengo letu ni kuwapa watoto, umahiri na maarifa ya muhimu ya kiustadi ya kuendeshea maisha, kutoa mafunzo maalumu kwa walimu na kuwawezesha kimaisha, kuhakikisha elimu bora na yenye thamani inatolewa kwa wanafunzi wote bila ya ubaguzi na kuhakikisha sekta ya elimu ya wananchi wa Libya inafufuka na inakabiliana vizuri na masaibu na machungu ya vita vya miaka mingi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live