Zaidi ya watu 176 wamefariki kutokana na mafuriko katika eneo la Kalehe, Kivu Kusini, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Katika mahojiano ya simu na Sauti ya Amerika VOA, Gavana wa Kivu Kusini Theo Ngwabidhe amesema kwamba idadi ya vifo huenda ikaongezeka kwa sababu bado shughuli ya uokoaji inaendelea.
Mvua kubwa imekuwa ikinyesha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu Alhamisi.
Maafa makubwa yametokea katika vijiji vya Bushushu, Kabushonge, Nyamukiba na Minova.
Kulingana na shirika moja la kutoa misaada, uharibifu mkubwa umetokea katika Kijiji cha Nyabmukiba.
Idadi kubwa ya waliofariki ni wanawake na Watoto. Gavana Ngwabidje ameambia Sauti ya Amerika kwamba shughuli ya uokoaji inaendelea.