Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliohusika na ufisadi fedha za corona kushtakiwa

B47ca9349d39f302aa6569167841603d Waliohusika na ufisadi fedha za corona kushtakiwa

Fri, 25 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAOFISA 15 wa ngazi za juu nchini Kenya na baadhi ya wafanyabiashara wanatarajiwa kuburuzwa mahakamani wakihusishwa na wizi wa mamilioni ya dola zilizotolewa kwa ajili ya kununua vifaa vya kukabiliana na covid-19.

Wachunguzi wamegundua jinsi zabuni za serikali zilivyotolewa kwa watu walio na uhusiano wa karibu na wanasiasa na wafanyabiashara kinyume na masharti ya zabuni nchini Kenya.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na Kamati ya Seneti ya Afya na Covid-19 pamoja na Kamisheni ya Maadili na Mapambano dhidi ya Rushwa (EACC), ilieleza kuwa uchunguzi ulibaini kosa la jinai kwa maofisa hao wa umma katika ununuzi na usambazaji wa bidhaa za dharura za covid-19 katika Mamlaka ya Usambazaji wa Matibabu ya Kenya (Kemsa) iliyosababisha matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kamisheni hiyo ya EACC ilipendekeza maofisa wote wa Kemsa washtakiwe pamoja na wa Wizara ya Afya kwa kuwa wanaamini wote wanahusika na sakata hilo.

Awamu ya pili ya uchunguzi italenga kampuni zilizonufaika na zabuni hizo isivyo halali.

Viongozi wa juu wa Kemsa walisema hawahusiki na tuhuma hizo, ambapo ofisa mtendaji mkuu na maofisa wengine wawili katika mamlaka hiyo, walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliahidi kulipatia ufumbuzi sakata hilo ili kubaini nini hasa kilichotokea.

Agosti 26, mwaka huu, aliagiza mamlaka za uchunguzi kukamilisha uchunguzi wake ndani ya siku 21, ambapo tayari muda alioutoa umeshapita.

Tayari Kamisheni ya EACC imewasilisha ripoti yake na kutoa mapendekezo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anayetarajiwa kutangaza kukamatwa kwa maofisa waliohusika na tukio hilo wakati wowote.

Mpaka sasa watu 37,000 nchini Kenya wamekutwa na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) huku watu 659 wakiripotiwa kufariki dunia. Watu zaidi ya 24,000 wamepona.

Chanzo: habarileo.co.tz