MAOFISA wa Polisi katika Mji wa Busia nchini Kenya, wamewakamata watuhumiwa nane wanaodaiwa kuhusika na vurugu zilizotokea Jumamosi katika ziara ya kisiasa ya Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto.
Watuhumiwa hao, wanatajwa kuwa miongoni mwa watu waliofanya fujo kwa kuruushia mawe msafara wa Ruto na kufunga barabara, jambo lililosababisha watu kadhaa kujeruhiwa pamoja na uharibifu wa mali yakiwemo magari yote yaliyokuwepo kwenye msafara.
Katika tukio hilo, inaelezwa kwamba msafara wa Ruto ulizuiwa na kundi la vijana katika eneo la Korinda yalipo makutano ya Barabara ya za Kisumu na Busia ambapo vijana hao waliweka vizuizi barabarani kwa kuchoma matairi kisha wakaanza kurusha mawe kwenye msafara huo na kusababisha vurugu kubwa.
Polisi wamewataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni Fredrick Okoth, Reuben Barasa, Moses Oridi, Friday Ouma, Michael Omondi Alwando, George Odongo, David Ouma, na Wejuli Shalmin ambao wapo mahabusu katika Kituo cha Polisi Busia wakisubiri kupandishwa kizimbani kusomewa mashtaka ya uharibifu wa mali, kufanya vurugu na kuvuruga amani.
Jeshi la polisi nchini humo, limewataka wananchi kuepukana na matukio ya uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais na wabunge unaotarajiwa kufanyika mwaka 2022.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Fred Matiangi amelaani vikali tukio hilo na kusema serikali kamwe haitavumilia kwa mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga amani katika mikusanyiko ya kisiasa kwa sababu wanasiasa na wafuasi wao nchini humo, wanayo haki ya kikatiba kufanya shughuli za kisiasa kwa amani.
Akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini humo, Matiang’i aliagiza kukamatwa kwa watu wote waliohusika na tukio hilo na kufikishwa mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo huku pia akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini humo kutenda haki wakati wa kutimiza majukumu yake.