Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliobaini kuwa watoto si wao wataka taarifa zifutwe

Dna Pic Waliobaini kuwa watoto si wao wataka taarifa zifutwe

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Takriban wanaume 32 wameiandikia Kurugenzi ya Udhibiti wa Uraia na Uhamiaji (DCIC) nchini Uganda, wakitaka kufutwa kwa hati za kusafiria za watoto baada ya matokeo ya DNA kuonyesha kwamba wao siyo wazazi halisi wa watoto hao.

Msemaji wa Wizara ya Masuala ya Ndani wa nchi hiyo, Simon Mundeyi ameieleza tovuti ya Daily Monitor kuwa wanaume hao walituma maombi na kupata pasipoti za wake na watoto wao, lakini baada ya kufanya vipimo vya DNA na kubaini watoto hao si wa kwao, sasa wamerejea wakitaka maelezo yao yaondolewe kwenye hati za kusafiria za watoto hao. Hata hivyo, Mundeyi amesema kuwa, DCIC hawawezi kufuta hati za kusafiria isipokuwa walalamikaji waende kwa Mamlaka ya Usajili wa Vitambulisho vya Kitaifa nchini humo ili kubadilisha maelezo yao.

DCIC inasema wanaume hao wamehamasishwa kufanya uchunguzi wa DNA kwa watoto wao kutokana na matukio ya hivi karibuni yaliyotangazwa kwenye vyombo vya habari kuhusu wenzao ambao waligundua kuwa watoto walio nao si wao. Mojawapo ya kesi za hivi karibuni nchini humo ni ya mwanamume anayefanya kazi Ulaya ambaye alipowapeleka watoto wake sita kwa uchunguzi wa DNA, matokeo yalionyesha kwamba hakuwa baba mzazi kwa watoto hao. Mwanamume huyo amekuwa akiwasomesha watoto wote sita katika shule za gharama kubwa. Mundeyi amesema kuwa mwanamume huyo alisukumwa kuwachukua watoto hao sita kwa uchunguzi wa DNA baada ya ugomvi mkali na mkewe ambaye aliwaeleza kuwa baadhi ya watoto hao si wake. Ingawa mke aliomba radhi kwamba alitoa kauli hiyo kwa hasira, mwanamume huyo aliendelea na uchunguzi wa siri wa DNA katika Kurugenzi ya Maabara ya Uchambuzi ya Serikali (DGAL). “Matokeo yalipotoka, aliyapinga lakini tulimshauri apeleke sampuli kwenye maabara nyingine. Alichukua baadhi ya sampuli hadi Kanada na nyingine Afrika Kusini na Sampuli zote zilithibitisha kwamba hakuna mtoto hata mmoja kati ya sita aliyekuwa wake," Mundeyi alisema. Makumi ya wanaume wamekuwa wakimiminika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakitaka kufanya vipimo hivyo kutaka kujua kwamba watoto walio nao ni wao au laa.

Chanzo: Mwananchi