Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limewashutumu walinzi wa mpakani wa Saudi Arabia kwa kuwaua mamia ya wahamiaji wa kiuchumi wa Ethiopia waliokuwa wakijaribu kuvuka kutoka Yemen yenye vita.
Wanasema takribani watu 655 wameuawa na walinzi tangu mapema mwaka jana.
Baadhi walipigwa risasi, wengine kuuawa au kulemazwa na silaha za vilipuzi.
Shirika hilo lilitumia miezi kadhaa kukusanya ushahidi, baada ya Umoja wa Mataifa kutoa madai kama hayo mwaka jana.
Human Rights Watch imeyataja mauaji hayo kuwa yameenea na ya kimfumo, na yanasema yanaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Mwezi Machi, serikali ya Saudia ilikataa kabisa pendekezo lolote kwamba vikosi vyake vilihusika katika mauaji ya kuvuka mpaka.