Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakutana kujadili fursa mataifa ya SADC

80684f6acb23281c7f148d4a4a25449b.jpeg Wakutana kujadili fursa mataifa ya SADC

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MTANDAO wa wakulima wa Afrika Mashariki na nchi za Kusini (ESAFF), umezikutanisha Asasi, taasisi za umma pamoja na wadau wa vyombo vya habari ili kuzungumzia fursa zinazopatikana katika mipango mikakati na dira za Juimuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano wa siku mbili uliofanyika kwa njia ya mtandao, uliandaliwa na mtandao huo kwa kushirikiana na Shirika la Wadhamini la Afrika Kusini (SAT) na Wakala wa Ujerumani wa Ushirikiano wa Kimataifa (GIZ).

Mratibu wa ESAFF, Joe Mzinga alisema lengo lao ni kujenga uwezo kwa wadau hao ili kujua dira ya SADC ya mwaka 2050 na mpango mkakati.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti washiriki hao akiwemo Mwakilishi kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Frank Dafa alisema ipo haja ya serikali kutengeneza mazingira wezeshi ya kufanya biashara na kuishukuru serikali kwa namna inavyoendelea kuboresha miundombinu.

Audax Lukonge kutoka Jukwaa la Wadau wa Kilimo nchini (ANSAF), alisema ipo haja ya kurasimisha mipango iliyowekwa na kuweza kufanyiwa kazi ikiwemo sera mbalimbali zilizokubaliwa na wanajumuiya.

Mojawapo ya sera hizo ni pamoja uondoaji wa tozo mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kwa watu waliowekeza katika sekta ya kilimo na kuangalia huduma za ugani na kilimo cha mkataba

"Pia hapa kuna haja ya kutekeleza ile sera ya kutenga asilimia 10 ya bajeti yake kupeleka kwenye kilimo na chambua faida na uzalishaji wa mazao ili kuwepo na tija," alisema.

Rebeca Muna kutoka Forum CC alisema kuna haja ya kuendelea kuwekeza zaidi kwenye tafiti ili kufikia malengo hayo yaliyowekwa.

Awali, wakiwakilisha mada kwa upande taasisi za serikali, Caroline Valerian kutoka Wizara ya Viwanda alisema serikali inategemea kuongeza hisa upande wa biashara na viwanda huku akieleza kuwa wamejipanga kutengeneza mazingira wezeshi kwa kuongeza tija upande wa uzalishaji bidhaa ikwemo chakula.

Dynes Mtei kutoka wizara ya Kilimo, alisema kupitia mpango wa maendeleo ya sekta ya kilimo(ASDP II), watauwezesha ili kuweza kufikia mpango wa SADC ikiwemo ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo wakulima.

Chanzo: www.habarileo.co.tz