Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakimbizi wa ndani watekwa nyara nchini Nigeria

Wakimbizi Wa Ndani Watekwa Nyara Nchini Nigeria Wakimbizi wa ndani watekwa nyara nchini Nigeria

Wed, 6 Mar 2024 Chanzo: Bbc

Makumi ya wakimbizi wa ndani walitekwa nyara mwishoni mwa juma na Boko Haram karibu na kambi ya Ngala, kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno.

Idadi kamili ya waathiriwa haijabainika, lakini baadhi ya ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinasema kuwa huenda ikafikia 319, na hivyo kufanya kuwa utekaji nyara mkubwa zaidi wa raia katika jimbo la Borno tangu kutekwa nyara kwa wasichana 276 kutoka Chibok mwaka wa 2014.

Kuna ripoti nyingi zinazokinzana kuhusu ni nini hasa kilitokea Ngala wikendi hii.

Hata siku ambayo waathiriwa walichukuliwa inabishaniwa, na vyanzo vya habari katika eneo hilo kutokubaliana ikiwa ilifanyika Ijumaa, Jumamosi au Jumapili.

Tunachojua ni kwamba wakimbizi wa ndani kutoka kambi ya Ngala, karibu na mpaka na Cameroon walitekwa nyara.

Wengi wanakadiriwa kuwa wanawake na wasichana ambao walikuwa wakiokota kuni ili kuuza na kutumia kupikia.

Viongozi wa wanamgambo wa eneo hilo wameliambia shirika la habari la AFP ni wanawake 47 pekee ambao bado hawajapatikana.

Mamlaka katika jimbo la Borno bado haijathibitisha idadi ya watu waliotekwa nyara.

Tukio hilo linakuja wakati serikali ya Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, ilisema kuwa 95% ya wapiganaji wa Boko Haram walikuwa wamekufa au wamejisalimisha kwa mamlaka.

Kwa zaidi ya muongo mmoja, wapiganaji wa Kiislamu wamekuwa wakifanya mashambulizi na utekaji nyara wa watu wengi kaskazini mwa Nigeria, na kuua zaidi ya watu 40,000 na milioni mbili kuyahama makazi yao.

Chanzo: Bbc