Wakimbizi wa ndani zaidi ya 60 wakiwemo watoto wadogo 33 wamepoteza maisha kutokana na njaa katika mkoa wa Kwilu, katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hayo yalisemwa jana Ijumaa na Kamisheni ya Masuala ya Kibinadamu ya Mkoa wa Kwilu na kuongeza kuwa, wakimbizi wapatao 4,600 waliotokea eneo la Kwamouth mkoani Mai-Ndombe na ambao hivi sasa wanaishi katika eneo la Bandundu mkoani Kwilu, wanasumbuliwa na uhaba wa chakula na mahitaji mengine ya msingi.
Frederic Nkumpum, mshauri mwandamizi wa asasi ya kiraia ya Kwilu Humanitarian Actions amesema vifo hivyo vya makumi ya wakimbizi wa ndani ya DRC vimeripotiwa tokea kundi la wakimbizi hao liwasili katika eneo la Bandundu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti.
Amesema: Kwa ujumla, watoto 33 na watu wazima 27 wakiwemo wanawake 17 na wanaume 10 wameaga dunia kutokana na njaa. Kuna tatizo la mazingira ya kuishi linalotokana na watu hawa kukosa misaada. Hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa juu ya namna watakavyopata chakula.
Nkumpum ameongeza kuwa, "Hapa Bandundu, idadi ya watu waliofurushwa makwao ni 4,669. Kwa hakika wanahitaji msaada wa dharura. Tunaendelea kutoa mwito kwa wafadhili na washikadau waje na kuwasaidia wakimbizi hao wanaoteseka."
Makundi ya wanamgambo na waasi wanaobeba silaha katika pembe mbalimbali za Kongo DR mara kwa mara yamekuwa yakiwashambulia raia na kuwafurusha kwenye makazi yao, na hata kushambulia katika kambi za wakimbizi.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 6.2