Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakimbizi wa Burundi wanaorejea kwao wawe mabalozi wa amani

A0ab577be52bf9cfdba8e621ee99ad47 Wakimbizi wa Burundi wanaorejea kwao wawe mabalozi wa amani

Tue, 29 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Rwanda, limesema wakimbizi wa Burundi 8,000 wamejisajili kurejea nchini mwao kwa hiari kati ya wakimbizi karibu 72,000 wanaoishi nchini humo.

Kwa kushirikiana na serikali ya Rwanda, wiki iliyopita kundi la tatu la wakimbizi 511 wa Burundi, waliondoka nchini humo kurejea nchini mwao kutoka kambi ya wakimbizi ya Mahama kupitia mpaka wa Nemba.

Takwimu za Wizara ya Kukabiliana na Majanga ya Rwanda, zinaonesha kuwa baada ya kulipuka kwa ugonjwa wa covid-19, kundi la kwanza la wakimbizi wa Burundi waliorejea nchini mwao walikuwa 485, kundi la pili wakimbizi 507 na kundi hilo la tatu wakimbizi 511 na wakimbizi wengine watarejea wiki hii.

Kabla ya Rwanda kufunga mpaka wake ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa covid-19, kati ya mwaka 2015 mpaka Machi mwaka huu, wakimbizi 5,922 walikuwa wameisharejea nchini Burundi kwa hiari.

Mbali na Rwanda, Tanzania akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri George Simbachawene alisema katika mwaka wa fedha 2019/2020 wamefanikiwa kuwarejesha kwa hiari yao wakimbizi 9,875 wa Burundi.

Inaelezwa kuwa tangu mwaka 2017, wakimbizi 89,000 walisaidiwa kurejea nchini Burundi, wengi wakitokea nchini Tanzania na wengine wachache wakitokea Kenya na DRC.

Ni dhahiri kuwa kasi ya wananchi wa Burundi kurejea kwa hiari nchini mwao, baada ya kuombwa na serikali ili kuunganisha nguvu katika ujenzi wa nchi yao umekuwa mkubwa, jambo linalodhihirisha kuwa amani na usalama wa Burundi umekuwa wa kuridhisha.

Serikali imesema itawasaidia kurejea katika maisha ya kawaida, ili kuwezesha ujenzi wa maisha yao. Pia serikali imesema itasaidia kuimarisha umoja na ushirikiano wa kujenga nchi hiyo iliyogubikwa na migogoro kwa muda mrefu.

Pongezi kwa wakimbizi, nchi na NHCR kwa kuwawezesha wakimbizi wa Burundi kurejea kwao kwani inaonesha upendo na undugu wa dhati, kwani hakika mkimbizi anaporejea kwao, anakuwa huru kuliko akiwa nchi ya ugenini kwenye makambi maalumu.

Ni vema kwa wakimbizi wanaorejea nyumbani, kuhakikisha wanakuwa baraka kwa serikali na jamii na si kusababisha vurugu na migogoro, ambayo serikali imejaribu kwa kiasi kikubwa kuiondoa na kuanza upya katika maendeleo ya nchi na wanachama wake.

Ni kweli wapo waliotengana na ndugu zao kwa muda mrefu na wengine wamepoteza maisha. Hata hivyo, hiyo isiwe sababu ya kutaka kulipiza kisasi, bali waanze pale walipo sasa na kuendelea na maisha.

Wakimbizi ambao ni raia wa Burundi, mchango wao unahitajika sana katika kukuza uchumi wa nchi yao, kwani kurejea kwao kutachochea maendeleo katika sekta mbalimbali za biashara na kilimo. Hivyo, kamwe wasikubali kuwa wachochezi wa vurugu na ugomvi katika nchi hiyo.

Wote tunatambua kuwa amani na usalama wa Burundi, unaelezwa na wakimbizi wenyewe wanaorejea kwao, kwa sababu hadi sasa hakuna anayeonekana kujutia uamuzi huo wa kurejea nchini mwao.

Wote tunatambua kuwa ‘Mkataa kwao ni mtumwa’ hivyo nawatakia kila la heri wananchi wa Burundi wanaorejea kwa hiari.

Chanzo: habarileo.co.tz