Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakimbizi 60,000 warejea Burundi kwa hiari

9a79e4185cd00bec477d60483ed87333 Wakimbizi 60,000 warejea Burundi kwa hiari

Tue, 2 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), limesema zaidi ya wakimbizi 60,000 wa Burundi wamerejea nyumbani kwa hiari mwaka huu na hivyo kumaliza miaka ya uhamishoni katika nchi tano jirani.

Kuchaguliwa kwa aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza (sasa ni marehemu) ili kuwania muhula wa tatu mwaka 2015 kuliibua wimbi kubwa la wakimbizi kutoka nchini hapa.

Serikali iliyopo madarakani sasa chini ya Rais Evariste Ndayishimiye imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuwashawishi wakimbizi wa Burundi kurejea nchini hapa kwa hiari.

Msemaji wa UNHCR, Shabia Mantoo alisema mpango wa usaidizi wa hiari wa wakimbizi kurejea, ulioanza mwaka 2017 na umekuwa ukishika kasi baada ya uchaguzi wa nchi hiyo mwaka 2020 uliomweka madarakani Ndayishimiye.

Msafara wa wakimbizi 343 wa Burundi ulirejea nchini kutoka Uganda mapema wiki iliyopita. UNHCR inaripoti takribani nusu ya idadi hiyo wamerejea kutoka Tanzania, huku wengine wakitoka Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya.

Kwa mujibu wa Mantoo, shughuli za kuwarejesha nyumbani wakimbizi zinaendelea kwa mtindo wa haraka na uliopangwa. Anasema misafara ya wakimbizi wapatao 1,500 hufika Burundi kila wiki.

"Wanapofika katika moja ya vituo vitano vya mapokezi, familia zinazorejea hupewa vifaa vya nyumbani na usaidizi wa pesa ili kuwasaidia kuanza upya maisha yao. Hata hivyo, usaidizi zaidi unahitajika ili kufikia ujumuishaji tena endelevu kwa watu hawa (ambao) wanarejea na pia kwa jamii nchini Burundi zinazowapokea. Mara nyingi miundombinu ya kijamii na kiuchumi inayohitajika hukosekana,” alieleza.

UNHCR inaripoti kuwa imepokea asilimia 10 tu ya Dola milioni 104.3 inazohitaji kusaidia kurejea na kuunganishwa tena nchini Burundi. Inabainisha kuwa, hili ni tatizo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokwenda nyumbani.

Tangu 2017, zaidi ya wakimbizi 180,000 wa Burundi wamerejea nyumbani kwa hiari. Hata hivyo, karibu wakimbizi 270,000 wa Burundi wamesalia uhamishoni.

Chanzo: www.habarileo.co.tz