Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakenya wawabana Ruto, Odinga muafaka wa kisiasa

Odinga And Ruto Wakenya wawabana Ruto, Odinga muafaka wa kisiasa

Tue, 11 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais William Ruto wa Kenya na kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, wako kwenye shinikizo la kubuni Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kurejesha utulivu wa kisiasa nchini Kenya.

Ripoti zinasema kuwa juhudi za kuwashawishi wawili hao kubuni handisheki na mapatano ya kisiasa kama yale yaliyobuniwa mwaka 2018 baina ya Bw Raila Odinga na Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta, zinaendelea kushika kasi.

Mwafaka baina ya viongozi hao wawili ulifuatia utata uliozuka kuhusu uchaguzi wa urais wa 2017.

Duru katika kambi za Rais Ruto na Bw Odinga zimeviambia vyombo vya habari kwamba katika kumaliza mzozo huo, huenda kukawa na masuluhisho mawili ambayo ni ama kubuniwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani au kuanzishwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Rais Ruto amelazimika kujitokeza hadharani kushinikiza kubuniwa kwa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani kupitia Bunge la Kitaifa ili kujaribu kumridhisha kiongozi wa kambi ya upinzani Raila Odinga. Lengo kuu la hili ni kumaliza mzozo huo na kuepuka hali ambapo huenda upinzani ukajumuishwa katika serikali yake.

Mzozo wa kisiasa umetokota nchini Kenya katika siku za hivi karibuni huku nchi hiyo ikitikiswa na maandamano ya ghasia yaliyoongozwa na kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga anayedai kwamba kulifanyika udanganyifu katika uchaguzi wa rais wa Agosti 22 mwaka jana.

Raila Odinga anasema atarudi kwa wananchi iwapo kutakuwa na dalili za kukosekana kwa umakinifu kutoka upande mwingine katika suala la mazungumzo ya mapatano na ametaka kufunguliwa sava za kura za uchaguzi wa rais huku Ruto akipinga suala hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live