Wakenya wamepewa likizo maalum ya kupanda miti milioni 100 kama sehemu ya lengo la serikali kupanda miti bilioni 15 katika kipindi cha miaka 10.
Likizo hiyo inaruhusu "kila Mkenya kumiliki mpango huo", kulingana na Waziri wa Mazingira Soipan Tuya.
Kila Mkenya anahimizwa kupanda angalau miche miwili, hivyo basi kufikia lengo la milioni 100.
Takriban miche milioni 150 imepatikana katika vitalu vya umma.
Serikali itakuwa ikitoa miche hiyo bila malipo katika vituo vya wakala wa misitu ili Wakenya waipande katika maeneo maalum ya umma.
Lakini pia imewahimiza Wakenya kununua angalau miche miwili ili kuipanda katika ardhi yao wenyewe.
Rais William Ruto anaongoza zoezi hilo eneo la Makueni mashariki mwa nchi. Mawaziri wametumwa katika mikoa mingine kuongoza shughuli hiyo pamoja na magavana wa kaunti.
Upandaji miti utafuatiliwa kupitia programu (app) ya mtandao, ambayo inafuatilia zoezi hilo kwa kuruhusu watu binafsi na mashirika kurekodi shughuli, ikiwa ni pamoja na aina ya mimea, nambari na tarehe iliyopandwa.
Programu ya Jaza Miti pia itasaidia watu kupanda miche inayofaa kwa kulinganisha eneo la ardhi na spishi zinazofaa, kulingana na wizara ya mazingira.
Bi Tuya aliaambia televisheni ya Citizen nchini humo siku ya Jumapili usiku kwamba muitikio uilikuwa "wa kushangaza" na tayari kulikuwa na usajili milioni mbili kwenye programu kufikia Jumapili.
Hata hivyo alisema upandani wa miche hiyo hautafanyika katika eneo la kaskazini-mashariki, ambako kumekuwa na mafuriko.
Kwa sasa nchi inakabiliana na mvua kubwa ya El NiƱo ambayo imeiwaua makumi ya watu, maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kuharibu miundombinu - huku eneo la kaskazini likiathirika zaidi.
Wakenya wameitikia kwa kiasi kikubwaupandaji miti huku pia wakibainisha baadhi ya changamoto.
Mwanamazingira Teresa Muthoni aliambia BBC kwamba mpango huo ulikuwa "wazo zuri sana", lakini zoezi hilo halikuandaliwa kwa njia ambayo ingehakikisha kila mtu yuko nje akipanda miti.
Alisema "watu wengi wanapaswa kuendelea na kazi zao za kuweka chakula mezani... inakuja wakati uchumi wetu hauendi vizuri hivyo watu wengi wanatatizika kifedha".
Pia alibainisha kuwa "miti mingi kati ya milioni 150 inayopatikana" katika vitalu vya umma ilikuwa ya migeni. "Ni muhimu sana kupanda miti inayofaa mahali pazuri," alisema.
Serikali pia imekosolewa kwa kutetea upandaji miti huku ikishindwa kudhibiti ukataji haramu wa miti katika misitu ya umma - hivi majuzi iliondoa marufuku ya ukataji miti.
Lakini siku ya Jumapili, waziri alitetea uamuzi huo, akisema ni misitu iliyotengenezwa kwa madhumuni ya kibiashara pekee ndiyo iliyoathiriwa - karibu 5% ya jumla ya misitu yote.