Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakenya kuamua rais wao leo

632639172360f61366a27b1369a93b1e.jpeg Wakenya kuamua rais wao leo

Tue, 9 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi wa Kenya leo wanapiga kura kuchagua viongozi mbalimbali akiwamo rais wa nchi baada ya Uhuru Kenyatta kumaliza muda wake huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikisema iko tayari.

Nafasi ya urais katika uchaguzi huu inawaniwa na Naibu Rais, Dk William Ruto kupitia Muungano wa Kenya Kwanza, Raila Odinga kupitia Muungano wa Azimio la Umoja, David Mwaure Waihiga kupitia Chama cha Agano na Profesa George Luchiri Wajackoyah.

Aidha, wagombea urais hao wamehitimisha kampeni zao kwa namna tofauti, watatu wakitumia ibada za Jumapili kumwomba Mungu washinde huku wakisisitiza amani.

Kampeni za mwisho nchini Kenya zilihitimishwa Jumamosi kwa wagombea wote wa urais kufanya mikutano mikubwa katika Jiji la Nairobi lenye idadi kubwa ya wapigakura.

Katika kuhitimisha, Ruto alitumia muda mwingi kujinasibu kama mwokozi wa vijana na wananchi masikini. Aliahidi kutengeneza ajira kwa vijana na kuhakikisha anashusha gharama za maisha alizosema zinawatesa Wakenya kwa sasa.

Mgombea urais huyo aliwaahidi wakulima na wafanyakazi nchini humo kuwa, endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Kenya, atafanya kilimo cha nchi hiyo kuwa chenye tija kwa kutoa ruzuku na fedha kwa wakulima.

Mgombea urais kupitia Umoja, Raila, katika kampeni zake aliahidi kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi serikalini na kuboresha usalama wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Raila Odinga ambaye pia aliwahi kufungwa jela mara kadhaa wakati alipokuwa akipigania demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya, aliahidi kuwawezesha kifedha watu masikini na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Wakenya wote.

Wagombea hao waliitumia Jumapili kwenda kanisani kufanya ibada na kuliombea taifa lao kupita salama katika uchaguzi huo.

Wagombea wote walitawaliwa na neno ‘amani’ katika midomo yao hali inayothibitisha kuwa wote hawako tayari kuona machafuko yakitokea katika uchaguzi huo jambo ambalo limepongezwa na wengi ndani na nje ya Kenya.

Ruto alifanya ibada katika makanisa matatu tofauti jijini Nairobi na alipotoka akapata nafasi kushiriki kipindi katika vituo viwili vya televisheni ambako kote alijitahidi kuwakumbusha Wakenya umuhimu wa amani.

Akiwa katika Kanisa la Mafunzo ya Yesu huko Kayole katika Kaunti ya Nairobi pamoja na Mgombea Mwenza, Rigathi Gachagwa, pamoja na Kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, Ruto aliwataka Wakenya kudumisha amani kabla, wakati wa kutangaza na kupokea matokeo na hata baada ya uchaguzi.

Kwa upande wa Raila, akiwa na Mgombea Mwenza, Martha Karua, walitumia siku hiyo kufanya ibada katika Ukumbi wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (KICC) jijini Nairobi. Wanasiasa hao waliwataka Wakenya kushiriki uchaguzi kwa amani na kuepuka vurugu.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya wanasema kitendo cha kuitumia siku ya Jumapili kusali katika makanisa kwa wagombea wa urais katika uchaguzi wa Kenya kinalenga kutuliza munkari walionao wapiga kura kuelekea katika uchaguzi huo.

KURA YA MAONI

Kura za maoni kwa ujumla wake zinamweka mbele Raila Odinga akifuatiwa kwa karibu na Ruto.

Kwa mujibu wa matokeo ya hivi karibuni yaliyotolewa na Kituo cha Demokrasia Afrika, kama Wakenya wangefanya uchaguzi Agosti 3, 2022 Raila angepata asilimia 47 ya kura zote huku Ruto akipata asilimia 41.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati alisema matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa ndani ya wiki moja baada ya upigaji kura kukamilika.

Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya ili kushinda moja kwa moja, mgombea anahitaji kupata zaidi ya nusu ya kura zote na angalau asilimia 25 ya kura katika zaidi ya nusu ya kaunti zote 47.

Iwapo hatapatikana mshindi wa moja kwa moja, uchaguzi wa marudio utafanyika ndani ya siku 30.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live