Baada ya serikali kuwasimamisha kazi maafisa 27 kutoka taasisi kumi na mbili waliosaidia kuachiliwa kwa sukari iliyokwisha muda wake ambayo ilikuwa imepangwa kuharibiwa mwaka wa 2018 , serikali inasema Wakenya hawakabiliwi na hatari kwa sasa.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei Jumatano alitangaza kwamba kusimamishwa kazi kumechochewa na wizara mbili, Hazina ya Kitaifa inayoongozwa na Njuguna Ndung'u na Uwekezaji na Biashara inayoongozwa na Moses Kuria ikisubiri kukamilika kwa uchunguzi wa kisa hicho.
Shirika la Viwango vya bidhaa nchini Kenya (Kebs) lilikuwa limeona kuwa mifuko 20,000 ya sukari haifai kwa matumizi ya binadamu na ikaagiza ibadilishwe kuwa ethanoli ya viwandani.
Lakini shehena hiyo badala yake iliingizwa sokoni kinyume na sheria. Akizungumza na mwandishi wa BBC Carol Robi, Waziri wa biashara na uwekezaji Moses Kuria anatolea ufafanuzi zaidi Sakata hilo pamoja na kuelezea taarifa kuwa pia kuna maziwa ya unga yaliyopitisha muda wa matumizi sokoni.