Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajue wagombea vinara Uganda

4a0157eb6b4e703f2f0f37dfae848055 Wajue wagombea vinara Uganda

Wed, 9 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UCHAGUZI wa Uganda utakaofanyika Januari 14 mwakani unaendelea kushika kasi huku wagombea 11 wakiendelea kunadi sera zao.

Katika uchaguzi wa urais wa Uganda, mgombea anapaswa kuvusha asilimia 50 ya kura zote katika raundi ya kwanza. Asipovusha, wagombea wawili wa kwanza huchuana tena katika uchaguzi wa marudio.

Katika wagombea hao 11, watano miongoni mwao wanatoka katika vyama mbalimbali vya siasa lakini sita ni wagombea binafsi.

Hata hivyo, miongoni mwa hao 11 ni wagombea wawili ndio wenye nguvu ambao ni Rais wa sasa, Yoweri Museveni anayegombea kwa mara ya sita na Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu Bobi Wine, mwanamuziki aliyeamua kugeukia siasa.

Wagombea wengine ni kijana wa miaka 24, John Katumba na Nancy Linda Kalembe, ambaye ni mgombea urais mwanamke pekee katika kinyang’anyirio hicho.

Wagombea wengine ni Waziri wa zamani wa Ulinzi, Henry Tumukunde na kamanda wa zamani wa kijeshi, Mugisha Muntu.

Wagombea wengine ni Norbert Mao, Joseph Kabuleta Kiiza, Patrick Amuriat Oboi, Fred Mwesigye na Willy Mayambala.

Ni nani Bobi Wine?

Robert Kyagulanyi Ssentamu au Bobi Wine alizaliwa Februaru 12 mwaka 1982. Mbali na siasa, Bobi Wine pia ni mwimbaji, mcheza sinema na mfayanyabiashara.

Katika kipindi kilichopita alikuwa mbunge wa jimbo la Kyadondo katika wilaya ya Wakiso katikati mwa Uganda.

Anagombea kupitia chama cha National Unity Platform (NUP).

Ssentamu alikulia katika mitaa ya uswahilini ya Kamwookya, kaskazini mashariki mwa jiji la Kampala.

Alisoma katika Shule ya Kitante Hill na kuhitimu mwaka 1996 kisha akajiunga na Shule ya Sekondari ya Juu ya Kololoa ambako alihitimu mwaka 1998.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere ambako alisomea muziki, uchezaji dansi na uigizaji na kupata shahada yake mwaka 2003.

Mwaka 2016, Ssentamu alirejea chuoni kusomea sheria katika Chuo Kikuu cha International University of East Africa (IUEA).

Ssentamu alianza muziki mwanzoni mwa miaka 2000. Baadhi ya vibao vyake vya mwanzo ni "Akagoma", "Funtula", na "Sunda" (alichomshirikisha Ziggy D). Ni vibao vilivyompatia umaarufu katika eneo hili la Afrika Mashariki.

Muziki wake umekuwa ukigusa midundo ya reggae, dancehall, na mapigo ya kiafrika (afrobeat), mara nyingi zikiwa na ujumbe wa kijamii na kisiasa kidogo.

Kwa kipindi cha miaka 15 ya muziki wake ameshatoa zaidi ya nyimbo 70. Kibao chake cha Kiwani alichokitoa mwaka 2016, ulitumika katika wimbo wa Disney.

Aprili 2017, Ssentamu alitangaza kugombea uchaguzi mdogo jimbo la Kyadondo. Kampeni zake za mlango kwa mlango zilivutia watu wengi ndani ya Uganda na nje na mwisho alimshinda mgombea wa chama tawala, Sitenda Sebalu.

Yoweri Museveni

Yoweri Kaguta Museveni ndiye Rais wa sasa Uganda ambaye anagombea tena urais. Amekuwa madarakani tangu Januari 29, mwaka 1986. Kwa sasa ndiye rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu kulinganisha na wenzake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Museveni aliyezaliwa Septemba 15 mwaka 1944, alishiriki katika vita vya 'kuikomboa' Uganda vilivyomuondoa madarakani Idi Amin (1971–79) na kisha vile vya dhidi ya Obote aliyewahi kufanya kazi chini yake akiwa ofisa usalama (1980–85).

Rais Museveni anaaminika kwamba ndiye aliyerejesha hali ya utulivu nchini Uganda pamoja na kunyanyua uchumi wa nchi hiyo baada ya kutumbukia katika muongo mmoja wa vita. Mbali na kunyanyua uchumi, mafanikio mengine yanayotajwa katika kipindi chake cha utawala ni Uganda kuwa moja ya nchi za kupigiwa mfano katika kupunguza maambukizi ya Ukimwi Afrika.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Museveni alichukuliwa na nchi za Magharibi kama kizazi kipya cha viongozi wa Afrika wenye mitazamo mizuri.

Hata hivyo, baadhi ya wapinzani wa Museveni wanadai kwamba uongozi wake ulishiriki vita isivyo halali ndani ya DRC. Pia uwepo wake madarakani wa muda mrefu umekuwa ukiwapa 'ukakasi' baadhi ya watu.

Museveni aliwahi kulaumiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kukataa upinzani kwa maana ya kuruhusu vyama vingi vya siasa na sasa analalamikiwa kwa kukataa kuwa na katiba inayoweka ukomo wa uongozi.

Alikotokea

Akiwa amezaliwa katika kijiji cha Ntungamo, Museveni anatokea katika kabila la Banyankole, moja ya makabila makubwa nchini humo baada ya lile la Baganda. Baba yake, Amos Kaguta, alikuwa mfugaji wa ng'ombe. Huyu ndiye pia baba wa mdogo wake Museveni aitwaye Caleb Akandwanaho ambaye anajulikana zaidi Uganda kama Salim Saleh. Dada yao anaitwa Violet Kajubiri.

Museveni alianzia elimu yake katika shule ya msingi ya Kyamate, kisha akajiunga na shule ya kati ya Mbarara kabla ya kumalizia masomo yake katika shule ya sekondari ya Ntare School.

Mwaka 1967, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania. Akiwa chuoni hapo, alisoma uchumi na sayansi ya siasa. Alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakiamini sana katika ujamaa wa Kimarxi (Marxist), huku akipendelea siasa za kimapinduzi.

Akiwa chuoni hapo alianzisha kundi la wanafunzi wanaharakati na pia aliongoza kundi la wanafunzi waliokwenda kuungana na wapiganaji wa Msumbiji kupitia chama cha FRELIMO ambako alipata mafunzo ya kupigana vita ya msituni.

Akiwa mwanafunzi wa mwanaharakati mashuhuri Afrika, hayati Walter Rodney, Museveni aliandika tasnifu iliyojikita katika mtazamo wa Frantz Fanon kuhusu mapinduzi dhidi ya ukoloni mamboleo.

Mwaka 1970, Museveni alijiunga na idara ya usalama wa taifa Uganda chini ya Dk Apolo Milton Obote.

Wakati Meja Jenerali Idi Amin alipochukua madaraka ya nchi Januari 1971 kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi, Museveni alikimbilia Tanzania pamoja na watu wengine ikiwa ni pamoja na Obote.

Chanzo: habarileo.co.tz