Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waislamu wajiandaa kuanza Mwezi Mtukufu

2c9ff5964c3b6449af8607899fc530cf Waislamu wajiandaa kuanza Mwezi Mtukufu

Tue, 13 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKATI Waislamu nchini wakitarajiwa kuanza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani leo au kesho, Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), limewataka wafanyabiashara za vyakula wamuogope Mungu kwa kutopandisha bei za vyakula na bidhaa nyingine.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Shehe Khamis Mataka, alisema jana kuwa mfungo utaanza baada ya mwezi kuonekana na kutangazwa na mamlaka husika kupitia kamati ya taifa ya kufuatilia mwezi.

“Kwa Mwislamu yeyote, maandalizi ya kwanza ya Mwezi wa Ramadhani ni kuuona mwezi na hatakiwi kutangaza, bali atoe taarifa kwa mamlaka husika ambazo ndizo zitatangaza,” alisema Shehe Mataka alipozungumza na HabariLEO.

Alisema baada ya kuuona mwezi muumini wa Kiislamu atatakiwa kujiandaa kwa kuingia kwenye Mwezi wa Ramadhani akiuchukilia kama chuo cha tabia njema.

Alisema jana ndio ilikuwa Mwezi 29 wa Shaaban na kwamba, endapo mwezi utaonekana leo Waislaam wataanza kufunga, lakini usipoonekana kesho ndio itakuwa Ramadhani kwa kuwa siku ya leo ndio itamalizia mwezi 30 wa Shabaan.

“Huu ni Mwezi Mtukufu wa Kuraani kwani ni kipindi cha Mfungo wa Ramadhani ndipo Kuraani iliposhushwa. Lakini pia, huu ni mwezi wa toba, ni mwezi wa kufanya yenye heri na ni mwezi wa kutoa kwa wenye nacho kuwasaidia wasio nacho,” alisema Shehe Mataka.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kutangaza bei elekezi ya vyakula katika kipindi cha Mwezi wa Ramadhani ili kuwasaidia watu wafunge bila taabu.

Alisema kwa kuwa Tanzania Bara bei hupangwa kutokana na bei za soko, wafanyabiashara wanapaswa kumuogopa Mungu na kuitumia Ramadhani kutenda wema kwa kutoongeza bei za bidhaa hususani zilizo mahususi kwa ajili ya Mfungo wa Ramadhani.

“Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kupata thawabu, nawasihi ndugu zangu fanyeni wema kwa kutopandisha bei za vyakula,” alisema Shehe Mataka.

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni sehemu ya nguzo tano muhimu kwa Waislamu dunia nzima na huitumia kufunga, kuswali, kutenda mambo mema lakini pia kusaidia wasiojiweza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz