Wahisani waliahidi jumla ya dola bilioni 2.4 Jumatano, zikiwemo ahadi mpya zatakriban dola bilioni moja kwa ajili ya Pembe ya Afrika iliyokumbwa na ukame wakati wa mkutano wa wafadhili uliofanyika katika makao makuu ya UN, lakini wakashindwa kufikia lengo la dola bilioni 7 zinazohitajika.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwaambia wafadhili kwamba ni lazima wachukue hatua sasa, ili kuzuia mzozo kugeuka na kuwa janga. "Hapana shaka kwamba hatua italeta mabadiliko yote," alisema.
Umoja wa Mataifa unasema dola bilioni 7 zinahitajika mwaka huu, kusaidia karibu watu milioni 32 nchini Ethiopia, Kenya na Somalia, ambao wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, baada ya mvua kukosekana kwa misimu mitano, na kusababisha ukame ambao haujawahi kushuhudiwa.
Huku mwaka ukikaribia nusu, Guterres alisema wamepokea asili mia 20 tu ya fedha zilizoahidiwa.
"Bila ya ufadhili wa haraka na mkubwa, shughuli za dharura zitasimama na watu watakufa," aliwaambia wafadhili.
Ahadi za Jumatano pamoja na pesa ambazo Umoja wa Mataifa tayari umepokea mwaka huu kwa pembe ya Afrika, ni jumla ya dola bilioni 2.4.