Jeshi la Wanamaji la Morocco limeokoa wahamiaji haramu 67 waliokuwa wanaghariki kwenye bodi ya plastiki iliyokuwa imejaza watu kupindukia, nje ya pwani ya kusini magharibi mwa nchi hiyo ya kifalme.
Shirika rasmi la habari la Morocco (MAP) limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, kati ya wahamiaji hao haramu alikuwemo pia mwanamke mmoja na watoto wadogo watatu. Wameokolewa na jeshi la majini la Morocco katika umbali wa takriban kilomita 100 kutoka pwani ya mji wa bandari wa Tarfaya wa kusini magharibi mwa Morocco.
Baada ya kupewa huduma ya kwanza, wahamiaji hao, ambao walikuwa ni kutoka nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara, walipelekwa kwenye bandari ya Laayoune jana Ijumaa, ambako walikabidhiwa kwa polisi maalumu wa Morocco kwa ajili ya taratibu za kawaida za kiutawala.
Tamaa ya kupata maisha mazuri barani Ulaya inawafanya baadhi ya watu wasioona mbalimbali kuhatarisha maisha yao na mara nyingine wanaishia kupoteza maisha hata kabla ya kufika wanakokusudia.
Wakimbizi wa Afrika wakiihaha jangwani kwa tamaa ya kutafuta maisha mazuri barani Ulaya
Siku chache nyumba serikali ya Libya ilitangaza habari ya kugunduliwa miili 27 ya wahajiri wa Kiafrika katika jangwa la magharibi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Tunisia.
Mohamed Hamouda, Msemaji wa Serikali ya Libya alithibitisha habari hiyo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Associated Press lakini hakutoa maelezo zaidi mbali na kusema kuwa, uchunguzi wa kubaini uraia wa wakimbizi hao unaendelea.
Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wahajiri hao walioaga dunia katika mazingira ya kutatanisha wakiwa jangwani kwenye mpaka wa Libya na Tunisia ni raia wa nchi za eneo la chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika.
Hali ya mamia ya wahajiri wa Kiafrika waliokwama katika eneo la mpakani mwa Tunisia na Libya inazidi kuwa mbaya baada ya serikali ya Tunisia kuwafukuza wahajiri hao kwenye mji wa Sfax, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.