Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahamiaji haramu 5 wa Burundi kortini

2fdbaa77f11716616fc4e7e801d11d85.png Wahamiaji haramu 5 wa Burundi kortini

Sun, 3 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

IDARA ya Uhamiaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imewakamata na kuwafikisha mahakamani wahamiaji haramu watano kutoka Burundi.

Watu hao waliingia nchini kinyume cha sheria na wengine 10 wamerejeshwa nchini kwao, kutokana na umri wao kuwa chini ya miaka 18.

Pia idara hiyo imemfikisha mahakamani mkazi wa Kata ya Nyihogo wilayani Kahama, Justina Makoye (47) kwa kosa la kumwajiri mtoto chini ya umri wa miaka 18. Mtoto huyo ni mhamiaji haramu kutoka Burundi na alikuwa akiuza vitumbua.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mratibu wa Idara ya Uhamiaji wilayani Kahama, Abdalah Mohamedi.

Alisema wahamiaji haramu hao, walikamatwa wiki iliyopita katika msakato wa kushitukiza katika maeneo mbalimbali wilayani Kahama. Ulifanywa ili kukabiliana na wimbi la wahamiaji hao wanaoingia nchini kwa njia za panya.

Akiwa mahakamani, Justina alikiri kosa na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miezi mitatu gerezani au kulipa faini ya Sh 500,000 ambazo alilipa.

"Mtoto tuliyemkamata tumemrejesha kwao nchini Burundi kupitia mpaka wa Kabanga akiwa pamoja na wahamiaji haramu wengine kumi waliokamatwa kwenye operesheni inayoendelea," alieleza Mohamed.

Mohamedi aliwataja wahamiaji haramu wengine waliokamatwa na kufikishwa mahakamani kuwa ni Rutimana Ramadhani (18) aliyekamatwa Desemba 23, mwaka huu huko. Alikamatwa maeneo ya Phantom mjini Kahama ambako alikuwa akifanya biashara ya kuuza matunda.

Wengine waliokamatwa ni Ndaishimiye Ernest, Nduwimana Daniel, Minan Adamu na Niyongabo Veniste. Wote walikamatwa Desemba 23 wakiuza vitumbua na mayai katika machimbo madogo ya dhahabu ya Mwime wilayani Kahama.

"Baada ya kutiwa hatiani, watuhumiwa wote wamehukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miezi mitatu gerezani ama kulipa faini ya shilingi 500,000 kila mmoja, wote walishindwa kulipa faini na wamepelekwa gerezani ambako wameanza kutumikia adhabu yao," alieleza Mohamed.

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga,Rashidi Magetta alisema operesheni hiyo itakuwa endelevu na lengo ni kuhakikisha hakuna mtu asiyekuwa raia wa Tanzania, anayeingia na kuishi nchini bila kufuata sheria.

Chanzo: habarileo.co.tz