Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahamiaji 34 kutoka Afrika watoweka baharini wakielekea Ulaya

Wahamiaji Wazama.jpeg Wahamiaji 34 kutoka Afrika watoweka baharini wakielekea Ulaya

Sun, 26 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wahamiaji wasiopungua 34 wa Kiafrika walitoweka siku ya Ijumaa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuelekea Ulaya kuzama baharini karibu na pwani ya Tunisia.

Hii ni ajali ya tano ya meli katika muda wa siku mbili, na kuongeza idadi ya watu waliopotea kufikia 67 huku kukiwa na ongezeko kubwa la boti za wahamiaji haramu zinazoelekea nchini Italia.

Walinzi wa pwani wa Italia walitangaza Alhamisi kwamba wamewaokoa takriban wahamiaji 750 katika operesheni mbili tofauti kwenye ukanda wa pwani kusini mwa nchi hiyo. Saa kadhaa baadaye watu wengine wasiopungua watano walifariki dunia na wengine 33 hawajulikani walipo baada ya kujaribu kuvuka bahari ya Mediterranean kuelekea Ulaya wakitokea Tunisia.

Jaji nchini Tunisia Faouzi Masmoudi amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa watu saba pamoja na watoto wachanga na watoto wengine walikufa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka katika pwani ya mji ya Sfax.

Afisa wa Gadi ya Kitaifa ya Ulinzi wa Pwani Houssem Jebabli, amesema walinzi wa pwani walisimamisha boti 56 zilizokuwa katika safari katika muda wa siku mbili kuelekea Italia na kuwazuia zaidi ya wahamiaji 3,000, wengi wao wakiwa wanatoka katika nchi za Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, wahamiaji wasiopungua 12,000 ambao wamefanikiwa kufika nchini Italia mwaka huu, waliingia kwa boti kupitia Tunisia, ikilinganishwa na watu 1,300 katika kipindi kama hicho mwaka 2022. Hapo awali, Libya ilikuwa sehemu kuu ya kivuko iliyokuwa ikitumiwa na wahamiaji kutoka Afrika.

Ukanda wa pwani wa mji wa Sfax umekuwa mashuhuri ukitumiwa na watu wanaokimbia umaskini na migogoro katika nchi za Afrika na Asia Magharibi na kujaribu kutafuta maisha bora katika nchi za Ulaya.

Mwezi uliopita, Rais Kais Saied wa Tunisia alisema katika maoni yaliyokosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu na Umoja wa Afrika kwamba uhamiaji wa watu kutoka Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara ni njama inayolenga kubadilisha muundo wa idadi ya watu wa Tunisia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live