Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahajiri zaidi ya elfu moja wa Kiafrika wawasili Uhispania

Wahamiaji Df Wahajiri zaidi ya elfu moja wa Kiafrika wawasili Uhispania

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zaidi ya wahamiaji elfu moja jana Jumamosi waliwasili katika Visiwa vya Canary vya Uhispania wakitokea Afrika, katika safari hatari ya baharini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Shirika la Msalaba Mwekundu linalosaidia kutibu wahamiaji, limetangaza kuwa boti ya mbao iliyokuwa na wahamiaji 320 iliwasili kwenye kisiwa cha El Hierro, ambayo ni sehemu ya Visiwa vya Canary nchini Uhispania.

Waokoaji wanasema hiyo ilikuwa mashua iliyojaza wahamiaji wengi zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Yapata wiki tatu zilizopita, mashua iliyokuwa imebeba wahamiaji 271 iliwasili katika Visiwa vya Canary.

Shirika la Msalaba Mwekundu limetangaza kuwa, Jumamosi ya jana wahamiaji 738 waliwasili katika kisiwa cha El Hierro, 98 katika kisiwa cha Tenerife na 150 katika kisiwa cha Gran Canaria.

Visiwa saba vinavyounda Visiwa vya Canary vya Uhispania vimekuwa kivutio kikuu cha wahajiri waomba hifadhi wanaoondoka Afrika kuelekea Ulaya.

Kuanzia mwanzoni mwa Januari hadi katikati ya mwezi huu wa Oktoba 2023, zaidi ya wahamiaji 23,530 wamewasili kwenye visiwa hivvyo, idadi ambayo imeongezeka kwa 80% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Ripoti zinaonyesha kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wahamiaji wasiopungua 1,000 wamefariki dunia wakiwa njiani kuelekea Visiwa vya Canary.

Mienendo ya ubaguzi wa rangi na sera za nchi za Ulaya za kukataa kuwapokea wahamiaji wa Kiafrika vimesababisha maafa mengi ya binadamu kwa wahamiaji hao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live