Tume ya Huru ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (CENI), imesema kuwa wagombea 24 akiwemo wa Rais wa sasa wa nchi hiyo, Felix Tshisekedi, wametangaza rasmi kuwa watagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajia kufanyika baadaye mwezi Desemba.
DW imeripoti kuwa miongoni mwa wagombea hao, wamo wapinzani wa zamani, wanaogombea kwa mara ya kwanza na wale walioshindwa katika chaguzi zilizopita, na hivyo kufanya uchaguzi huo kuwa na idadi kubwa ya wagombea ambao wachambuzi wanaamini huenda wakagawanya kura za upinzani na kuimarisha nafasi ya ushindi kwa Tshisekedi.
Tume hiyo ya uchaguzi, imechapisha wasifu wa wagombea hao 24 katika akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa X ambao awali ulijulikana kama Twitter. Mahakama ya kikatiba itathibitisha rasmi orodha ya mwisho katika wiki zijazo.
Wakati huohuo, Tresor Kibangula, mchambuzi wa kisiasa katika kituo cha utafiti cha Ebuteliu, amesema mazungumzo yanaendelea miongoni mwa baadhi ya wagombea kuhusu kuungana na kumuunga mkono mpinzani mmoja maarufu.