Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagner: Mali yasitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine

Wagner: Mali Yasitisha Uhusiano Wa Kidiplomasia Na Ukraine.png Wagner: Mali yasitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine

Mon, 5 Aug 2024 Chanzo: Bbc

Mali inasema imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine, baada ya afisa wa kijeshi kusema kuwa Kyiv ilihusika katika mapigano makali karibu na mpaka wa Algeria mwezi uliopita.

Makumi ya wanajeshi na mamluki wa Mali kutoka kundi la Wagner la Urusi waliuawa katika mapigano ya siku kadhaa na waasi wa Tuareg wanaotaka kujitenga na wapiganaji wanaohusishwa na al-Qaeda.

Andriy Yusov, msemaji wa idara ya ujasusi ya jeshi la Ukraine, alisema wiki iliyopita kwamba waasi walipewa "taarifa muhimu" ili kutekeleza mashambulizi hayo.

Afisa wa ngazi ya juu wa Mali, Kanali Abdoulaye Maiga, amesema serikali yake ilishtushwa kusikia madai hayo na kuishutumu Ukraine kwa kukiuka mamlaka ya Mali.

Matamshi ya Yusov "yalieleza kuhusika kwa Ukraine katika shambulio la kuogofya, la kisaliti na la kinyama la makundi ya kigaidi yenye silaha" ambalo lilisababisha vifo vya wanajeshi wa Mali, ilisema taarifa ya Kanali Maiga.

Mali imeamua kuvunja uhusiano "ikiwa ni hatua ya haraka", alisema.

Wiki iliyopita, jeshi la Mali lilikiri kuwa limepata hasara "kubwa" wakati wa mapigano ya siku kadhaa ambayo yalizuka tarehe 25 Julai.

Mapigano hayo yametokea katika jangwa karibu na Tinzaouaten, mji wa kaskazini-mashariki kwenye mpaka na Algeria.

Ripoti zinasema kuwa wanajeshi hao wa Mali na Urusi walishambuliwa na waasi wa Tuareg na wapiganaji wa kundi tanzu la al-Qaeda, Jamaat Nusrat al-Islam wal-Muslimin wakati wakisubiri kuongezwa nguvu, baada ya kuondoka Tinzaouaten.

Si wanajeshi wa Mali wala Wagner, ambao tangu wakati huo wamejiunga na kundi linaloitwa Africa Corps, ambao wametoa takwimu kamili, lakini makadirio ya vifo vya wapiganaji wa Wagner ni kati ya 20 hadi 80.

Chanzo: Bbc