Wafungwa na mahabusu nchini Kenya, sasa wanaweza kuhudhuria maziko ya wanafamilia wa karibu, ikiwa hakuna sababu za msingi za kuwanyima haki ya kufanya hivyo.
Jaji Lawrence Mugambi amesema wafungwa wote waliohukumiwa na wafungwa wanaoshikiliwa chini ya ulinzi wana haki ya kutendewa utu.
Haki hii alisema ni pamoja na kuwaruhusu kuhudhuria mazishi ya wanafamilia wao wa karibu isipokuwa kama kuna sababu za msingi za kukataa kutoa ruhusa.
Hatua hii, ni kufuatia kesi iliyowasilishwa na mwanahabari wa zamani Moses Dola, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela mwaka wa 2018 kwa madai ya kumuua mkewe.
Dola aliwasilisha ombi hilo kufuatia kifo cha mama yake, ambapo alinyimwa fursa ya kuhudhuria mazishi yake, hatua aliyoiita ukiukaji wa uhuru wa kimsingi na haki za wafungwa.
Mahakama hiyo pia iliagiza Serikali kuweka kanuni zitakazoamua wafungwa ambao wamenyimwa haki zao za kuhudhuria mazishi ndani ya miezi sita ijayo.