Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara EAC kuja na sera ya pamoja ya biashara

5e9af422a879fa9126cd08961e26e53a Wafanyabiashara EAC kuja na sera ya pamoja ya biashara

Tue, 16 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BARAZA la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kwa kushirikiana na Shirikisho la Viwanda la Ujerumani (BDI) limeitisha wataalamu wa biashara na sera kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ajili ya kupanga orodha ya ajenda ya pamoja ya utetezi wa sera, inayolenga kuchochea biashara ndani ya EAC hadi kufikia asilimia 30.

Mkurugenzi Mtendaji wa EABC, Dk Peter Mathuki alisema hayo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa janga la ugonjwa wa Covid-19, limevuruga minyororo ya biashara kikanda na duniani na kusababisha kupungua kwa biashara ndani ya EAC.

Alisema kupungua kwa biashara, kumeongeza gharama za ufanyaji biashara hadi dola za Marekani bilioni 37 na kusababisha hasara ya pato la dola za Marekani bilioni 79 katika kanda hiyo.

"Janga la Covid-19 limeilazimisha EABC kuangazia tena na kuweka upya mipango ya utetezi wa sera kuelekea uthabiti wa uchumi na kusaidia mwendelezo wa biashara," alisema.

Dk Mathuki alisema usafirishaji wa bidhaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ulipungua kwa asilimia 4.7 hadi dola za Marekani bilioni 14.0 mwaka 2018 kutoka dola bilioni 14.7 mwaka 2017. Usafirishaji wa ndani ya EAC ulikuwa asilimia 22.4.

Alisema upungufu wa biashara kwa eneo la EAC, uliongezeka kwa asilimia 39.4 hadi dola za Marekani bilioni 24.3 mwaka 2018 kutoka dola bilioni 17.4 zilizosajiliwa mwaka 2017; na kwamba hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya biashara na uwekezaji ya EAC 2018.

"Ipo haja ya kuzungumza kwa sauti moja gharama za biashara wakati jamii ya wafanyabiashara inaimarisha juhudi za utetezi katika kupunguza athari za janga hilo kwa wafanyabiashara na kuchochea biashara ya ndani ya EAC hadi asilimia 30," alisema.

Aidha, Dk Mathuki alisema ipo haja ya kuondoa vizuizi visivyo vya ushuru (NTBs), na utekelezaji wa utaratibu wa usuluhishi wa mizozo ya kibiashara na uoanishaji wa ushuru wa ndani katika kanda, ambayo ni Ajenda ya Sera ya EABC 2021/22 inayolenga kukuza biashara na uwekezaji wa ndani ya EAC.

"Jitihada za utetezi zinahitajika ili kuharakisha kukamilika kwa ukaguzi kamili wa ushuru wa pamoja na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kukuza ukuaji wa viwanda na minyororo ya thamani,” alisema.

Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama, Malighafi na Nafasi katika Shirikisho la Viwanda la Ujerumani (BDI), Mathias Wachter alisema shirikisho hilo linaona uwezekano mkubwa wa ushirikiano baina ya sekta binafsi barani Afrika na Ujerumani.

Wachter alisema kutokana na janga la Covid-19 kunahitajika mageuzi ya kiuchumi, mwitikio wa usawa na sera bora za biashara.

"Kuimarisha ushirikiano kati ya Baraza la Biashara la Afrika Mashariki, Vyama vya Biashara vya Kitaifa na taasisi za biashara katika eneo hili ni muhimu katika kuelekea kuoanisha mipango ya utetezi wa sera inayoonesha changamoto za kibiashara zinazopatikana katika ngazi ya kitaifa," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz