Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachumi: Bomba la mafuta ushindi wa kiuchumi EAC

3293234a72b16e31352d6ed4d0ac1729 Wachumi: Bomba la mafuta ushindi wa kiuchumi EAC

Tue, 20 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KUSAINIWA kwa mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kumeelezwa kuwa ni ushindi mkubwa wa kiuchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya kukumbana na vikwazo vingi vilivyokuwa na lengo la kuzuia utekelezaji wake.

Hayo yalisemwa na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi na siasa kutoka nchi za Afrika Mashariki wakati wakijadili faida na changamoto za mradi huo katika Kipindi cha Maoni mbele ya Meza Duara cha Idhaa ya Kiswahili ya DW ya nchini Ujerumani.

Wachambuzi hao walisema mradi huo ulikumbana na vigingi vingi vilivyowekwa na wanaharakati wa mazingira na utawala bora ambao waliziandikia barua benki zote zilizoombwa kudhamini mradi huo wakihimiza kuacha kutoa fedha kwa kisingizio cha kulinda mazingira na utawala bora.

Mwenyekiti wa mjadala huo na mwandishi mkongwe kutoka Kenya, Josephat Charo alisema katika barua ya wanaharakati hao wameorodhesha madai kadhaa ambayo kama yangekubaliwa yangekwamisha utekelezaji wa mradi huo mkubwa.

Alisema baadhi ya wanaharakati walikuwa wakitoa madai kuwa, mradi huo utaleta hatari kubwa ya uharibifu wa mazingira na kwamba nchi washirika hazina rekodi nzuri ya haki za binadamu, utaharibu makazi asilia ya watu na uzalishaji wa hewa ya ukaa inayopingwa duniani kote.

Alisema pamoja na juhudi za wanaharakati hao kwa jumuiya ya kimataifa na katika benki zote zilizombwa kudhamini mradi huo, Afrika Mashariki imepata ushindi mkubwa wa kibiashara na uwekezaji kutokana na kukataliwa kwa hila za wanaharakati hao.

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi na siasa, Nassoro Kitunda kutoka Moshi alisema kinachotakiwa ni nchi zote za Afrika Mashariki kuwa kitu kimoja kupata ushindi wa kiuchumi wa jumla kwa sababu juhudi za kuukwamisha mradi huo zinaonyesha Afrika Mashariki ipo katika vita vya kiuchumi.

“Linapokuja suala la miradi mikubwa Afrika Mashariki na barani Afrika kwa ujumla limekuwa suala la kupingwa kwa nguvu zote na watu wanaojiita watetezi wa mazingira na haki za binadamu, lakini cha ajabu ni kuwa hawaoni kuwa miradi hiyo inaenda kujenga heshima na utu wa mwanadamu,” alisema.

Kitunda alisema kiuhalisia ni watu na mataifa ambayo hayalitakii mema bara la Afrika ndio wanaofanya juhudi za kukwamisha miradi ya kimkakati yenye manufaa makubwa kwa wananchi.

“Hata Tanzania ilishapitia katika sekeseke kama hilo kupitia miradi yake ya umeme kama wa Julius Nyerere katika Mto Rufiji ambao ulipingwa bila sababu za msingi,” alisema.

Alisema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ndizo zinazoongoza barani Afrika katika kutunza mazingira, lakini inapotokea zinataka kutumia sehemu kidogo ya ardhi yake kujiletea maendeleo kunazuka upinzani mkubwa kutoka nje kupinga miradi hiyo hali inayothibitisha kuwa ni vita ya kiuchumi.

Maur Bwana Maka ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi na siasa kutoka Kenya, alisema ingawa kiujumla inasemwa Afrika Mashariki imepata ushindi wa kiuchumi, lakini kiuhalisia Tanzania ndiyo iliyopata ushindi huo.

Alisema Wakenya wengi walikuwa na uhakika wa kushinda juhudii za kuishawishi Uganda ili bomba hilo liweze kupitishwa nchini kwao badala ya Tanzania kutokana na ukweli kuwa ni karibu zaidi kutoka Hoima hadi Bandari ya Kisumu (km 1,100) kuliko Hoima hadi Tanga zaidi ya kilomita 1,445.

“Ni katika muktadha huo Wakenya wanashangaa kuwa Uganda imetumia busara gani kupitisha mradi huo nchini Tanzania.”

“Kwa hakika kilichoibeba Tanzania ni amani na utulivu ikilinganishwa na eneo la Kaskazini mwa Kenya pamoja na hisani kubwa ambayo Tanzania ilifanya kwa Uganda kipindi cha Mwalimu Nyerere,” alisema Maka akiwa Mombasa.

Mwandishi mkongwe na mchambuzi wa masuala ya uchumi Uganda, Ali Mutassa alisema isingekuwa rahisi kwa wanaharakati kufaulu kutokana na kiwango cha fedha kilichowekwa na kampuni za mafuta na serikali zenyewe kwani ni kuwa kikubwa mno.

“Mfano, dola za Marekani bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa bomba pekee kwa ajili ya kusafirisha mafuta pamoja na dola bilioni 5 kwenda kwa mwenyeji Uganda kwa mujibu wa makubaliano katika mkataba,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz