Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji waliotoka Kenya wala `bata’ Bara

002c47f1d26bffbb3cee2893bc43291e Wachezaji waliotoka Kenya wala `bata’ Bara

Tue, 29 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WACHEZAJI wawili waliokuwa wakicheza soka nchini Kenya, Joash Ònyango `Ukuta wa Berlin’ na David Mapigano, wanafurahia maisha katika Ligi Kuu Tanzania Bara tangu walipotua nchini mwezi uliopita.

Mkenya Onyango ambaye ni nahodha msaidizi wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars na Mapigano, wanazichezea timu za Simba na Azam FC, ambapo walipokuwa Kenya wanadaiwa walikuwa wakisotea mishahara na stahiki zao nyingine, lakini sasa wanakula ‘bata’.

Wakati Mapigano sasa anacheza soka nchini kwao Tanzania baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na Azam Agosti mwaka huu, Onyango alisaini kwa mabingwa mara 21 wa Tanzania Bara, Simba, naye pia ana furaha tangu awasili nchini.

Kwa mujibu wa mtandao wa Nation, tofauti na Kenya ambako Ligi Kuu bado haijaanza kutokana na mlipuko wa janga la virusi vya corona, Ligi Kuu ya Tanzania na za nchi nyingine zilianza mwezi uliopita.

Tayari mechi nne zimekwishachezwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Tangu alipojiunga na Simba SC, Onyango, amecheza mechi zote za kirafiki na ameanza katika mechi zote nne za ligi.

Beki huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kilichoifunga timu iliyopanda daraja ya Ihefu FC 2-1 katika mchezo wa kwanza wa msimu, kabla ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Vijana hao wa kocha Mbelgiji Sven Vandenbroeck baadae waliisambaratisha Biashara United inayofundishwa na kocha Mkenya, Francis Baraza, 4-0 na kushinda 3-0 dhidi ya Gwambina FC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Onyango, ambaye pia aliwahi kuichezea Western Stima, alikuwa sehemu ya safu ya ulinzi ya Simba inayoundwa na Shomari Kapombe na Mu-Ivory Coast, Pascal Wawa.

Wameruhusu mabao mawili kuingia langoni mwao katika mechi nne walizocheza hadi sasa.

Mbali na kuishi eneo la Mbezi Beach ambako amepewa na gari, mfanyakazi na dereva, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 amekuwa akipanda ndege kila Simba inapocheza nje ya Dar es Salaam.

Pale Azam FC, Mapigano naye ameendeleza rekodi ya kutofungwa katika mechi nne walizocheza hadi sasa.

“Siwezi kusema kuwa niko katika kiwango changu bora kabisa, lakini mambo yamekuwa mazuri hapa kuliko nilivyokuwa Gor Mahia. Mshahara napata kwa wakati na hapa hakuna matatizo mengine nje ya uwanja,” alisema Mapigano

Chanzo: habarileo.co.tz