- Nasra alithibitishia kuwa karamu hiyo ilihudhuriwa na watu wa familia pekee kwa sababu ya sheria za COVID 19
- Pia alielezea kuwa sherehe kuu itaandaliwa baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadan
- Wavunja mbavu hao walikutana wakati wa kutafuta nafasi kwenye shoo ya Churchill mwaka 2018
- Rashid Abdalla alimvisha Nasra pete ya uchumba mnamo Februari 2021
Wachekeshaji wa shoo ya Churchill Nasra Yusuf na Rashid Abdalla siku ya Jumapili, Aprili 25, walifunga pingu za maisha katika hafla ya faraghani.
Nasra alithibitishia Tuko.co.ke kuwa karamu hiyo ilihudhuriwa na watu wa familia pekee kuafikiana na sheria ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19.
"Ndiyo ni kweli, tuliamua kufanya sherehe ndogo ya Nikkah kwa sababu ya janga," alisema.
Hata hivyo, alisema sherehe kuu itaandaliwa baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadan.
Wavunja mbavu hao walikutana wakati wa kutafuta nafasi kwenye shoo ya Churchill mwaka 2018 na wamekuwa wakichumbiana hadi Februari 2021 wakati Abdalla alimvisha Nasra pete ya uchumba.
"Nilisema ndiyo kwa kipenzi cha maisha yangu.....rafiki yangu wa dhati!.. nakupenda kila wakati," Nasra alitangaza kuvishwa pete kwenye Instagram.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na mchekeshaji maarufu Daniel Ndambuki alimaarufu Churchill, Nasra alihadithia namna wazazi wake walitaka kumuoza kwa mzee anayemzidi umri akiwa msichana mdogo.
"Baba yangu alikuwa ameamua kunioza, sasa akaleta mzee nyumbani. Nilikuwa naona mvi kwenye kichwa chake. Mama aliniomba kuvumilia akidai kuwa mzee huyo ana miaka michache tu ya kuishi," alisema.
Hata hivyo, mrembo huyo alikataa na kushikilia kwamba anataka kufuata ndoto zake na kuwa mwanamke aliyefanikiwa mashani.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.