Wabunge wanaoegemea mrengo wa Azimio nchini Kenya, wameondoka katika majengo ya Bunge wakati ambapo Waziri wa Fedha, Prof. Njuguna Ndung’u alipoanza kusoma bajeti ya mwaka 2023/2024.
Wabunge hao wanasema wameamua kuchukua hatua hiyo wakipinga jinsi muswada wa fedha ulivyopitishwa Bungeni jana (Juni 14, 2023), licha ya kufahamu kwamba wangeupigia kura tena, juma lijalo.
Muswada huo, ulijadiliwa na kusomwa mara ya pili hapo jana Jumatano, ambapo wabunge walivutana kuhusu baadhi ya vipengele, licha ya Serikali kukubali kufanya marekebisho katika baadhi ya vipengele vyake.
Miongoni mwa vipengele vinavyopingwa, ni pamoja na kodi ya ujenzi wa makazi nafuu, nyongeza ya kodi katika mafuta na bidhaa nyingine ambazo zinamgusa mwananchi moja kwa moja, lakini Serikali inasisitiza kuwa muswada huo lazima upitishwe.