WABUNGE wa upinzani nchini Uganda wamesusia vikao vya bunge wakidai serikali iwaachie wanasiasa wa upinzani ambao walikamatwa wakati wa kapeni za uchaguzi na baada ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge mwaka 2021.
Hilo limejiri hapo jana katika kikao cha bunge baada ya naibu Spika wa bunge kuwataka wasubiri hadi wiki ijayo.
Kulingana na mwandishi wa BBC Issaac Mumena, karibu wabunge wote wa vyama vya upinzani nchini Uganda waliondaka jana kwenye kikao cha bunge huku wakiwa wanaimba nyimbo za kutaka serikali kuwachia huru wafungwa wa kisiasa, na kupinga serikali inavyoendelea na unyanyasaji wa watuhumiwa kwa kuwaweka korokoroni baadhi yao bila kufikishwa mahakamani.
Kiongozi wa wabunge wa upinzani bungeni Mathias Mpuuga alipingana na Naibu Spika Anita Among alipotoa ripoti ya kupotea kwa watu na wengine kuzuiliwa bila kufunguliwa mashitaka na kuteswa.
Alitaka bunge kuzungumzia swala hilo lakini naibu Spika akawafahamisha mpaka wiki ijayo kwa kuwa anachukua hatua ya kumuelezea Spika.
Wabunge wa upinzani wanadai hawawezi kuendelea kuhudhuria vikao vya bunge wakati wenzao wanateswa magerezani
Baadhi ya wabunge wa chama tawala cha NRM waliobaki bungeni waliwalaumu wenzao wa upinzani kwa kutoka nje kwani na wao hawafurahishwa na vikosi vya usalama kuwatesa watuhumiwa.
Kwa upande wao ingekuwa bora zaidi kama wangesubiri siku ya Jumanne wiki ijayo kama walivyoshauriwa na naibu Spika.
Waziri wa mambo ya ndani wa Uganda alikanusha ripoti ya kuteswa watuhumiwa na kusema anakwenda kutowa ripoti siku ya Jumanne wiki ijayo.
Mwaka jana Rais Museveni aliwaonya walinda usalama na kuwataka kuacha kuwatesa watuhumiwa ili kusema wanachotaka, lakini bado vitendo vya unyanyasi wa watuhumiwa vinaendelea.
Hivi karibuni mwandishi wa vitabu na mwana harakati wa kutetea haki za binadamu Kakweza Rukirabashaija alilalamika mahakamani jinsi alivyoteswa na kikosi cha kumlinda Rais alipokamatwa, na madaktari wa Idara ya magereza walithibisha kuteswa kwake walipotakiwa na mahakama kufanya uchunguzi.