Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge EALA wataja dawa mivutano ya biashara EAC

680c81c9748f51ff2077d4e455f58576 Wabunge EALA wataja dawa mivutano ya biashara EAC

Tue, 6 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WABUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania wametaka kutekelezwa kwa Itifaki ya Umoja wa Forodha kwa kuundwa kwa kamati ya biashara ya EAC.

Aidha, wametaka kutengenezwa mfumo wa kusimamia bidhaa ili kuepuka migogoro ya ufanyaji biashara kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo. Wamesema hatua hiyo itasaidia kutatua migogoro kama ilivyo sasa ya Kenya kupiga marufuku uingizaji wa kutoka Tanzania na Uganda na kusababisha changamoto mbalimbali.

Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Dk Abdullah Makame akizungumza na gazeti hili, alisema ili kuzuia mivutano, ni lazima kuunda kamati hiyo iliyo katika ibara ya 24 ya utekelezaji wa Itifaki ya Forodha ya EAC.

Alisema kamati hiyo ambayo imekuwa ikijadiliwa katika vikao vya mawaziri itahusisha wataalamu watatu kutoka kila nchi wakiwemo wanasheria, wataalamu wa biashara na forodha kutoka kila nchi.

“Hili linahusisha nchi wanachama kwa kila moja kuhakikisha anakuwa na watu hao ambao watasimamia utekelezaji wa biashara kwa mujibu wa sheria na itifaki za EAC,” alisema na kuongeza kuwa kamati hiyo itasaidia katika utatuzi wa vikwazo vya kibiashara.

“Ni ngumu kushughulikia suala hili kama hakuna kamati hii ambayo ipo kwenye itifaki kwa miaka mingi lakini kwa muda wote mawaziri wamekuwa wakijadili katika vikao vyao bila utekelezaji,” alisema.

Dk Makame alisema suala jingine ni kutekelezwa kwa mfumo wa kusimamia ubora na usalama wa bidhaa za mimea, samaki, kuku na nyinginezo kwa kuwa na itifaki itakayosimamia ubora unaostahili.

“Mifumo hiyo EAC itakuwa na itifaki ya kusimamia ubora wa bidhaa ambapo tayari majadiliano yalifanyika na kuidhinishwa na nchi zote wanachama kasoro moja ambayo ilikwamisha kuendelea kwa mchakato.”

Alisema katika utekelezaji wa Umoja wa Forodha, moja ya malengo ni kutengeneza soko la ndani la EAC ili kuweza kujilisha wenyewe na kutokana na kuwa Tanzania ni kubwa imekuwa ikipata fursa ya kuuza mazao yake katika nchi za EAC.

“Lakini kumekuwa na sera mbovu zinazotesa nchi nyingine zinazotegemea chakula cha EAC lakini pia na wakulima wanaolima na kutumia gharama kubwa wakijua kuna soko la kutosha lakini mara nyingi ikifika wakati wa mavuno kunakuwa na zuio la kusafirisha chakula kwa madai ya usalama wa chakula,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz