Vyombo vya habari vya Algeria vilitangaza jana kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wanaopambana na ugaidi, siku ya Jumamosi waliua magaidi wawili karibu na mpaka wa kusini mwa nchi hiyo.
Wizara ya Ulinzi ya wa Taifa ya Algeria imetangaza habari hiyo katika ripoti yake maalumu na kuongeza kuwa: Ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na ugaidi na sambamba na kushukuru maafisa wetu wa upelelezi, wanajeshi wetu mashujaa wamefanikia kuua magaidi wawili, kujeruhi na kuwakamata wengine wawili wakati wa shambulio la kushitukiza lililofanywa Jumamosi.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Algeria imeongeza kuwa,: "Wanajeshi wetu pia wamekamata silaha nzito kama vile bunduki na vitu vingine katika opereseheni hiyo.
Licha ya kuimarika hali ya usalama nchini Algeria ikilinganishwa na miaka ya 1990, lakini mapigano yameendelea kushuhudiwa hapa na pale kati ya wanajeshi na magenge ya kigaidi hususan kwenye maeneo ya mashariki na kusini mwa nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.
Algeria inapakana na nchi za Mali na Niger upande wake wa kusini kama ambavyo inapakana na Libya upande wake wa mashariki, nchi ambazo zote kwa miaka mingi sasa zinaishi katika hali isiyo na utulivu wa kisiasa na kiusalama kutokana na mashambulio ya mara kwa mara ya magenge ya kigaidi.