Kamanda wa jeshi la Uganda, UPDF Meja Generali Dick Olum amesema operesheni ya kuwaokoa wanafunzi waliotekwa nyara imeanza.
Ameongeza kuwa wametuma ndege za kutafuta na kuwakoa wanafunzi waliochukuliwa baada ya tukio la uasi linaloshukiwa kufanywa na kundi la ADF.
Kulingana naye, baadhi ya wanafunzi, haswa wavulana waliteketezwa hadi kufa huku wasichana wakikatwakatwa na wengine kuchukuliwa mateka.
Ameyasema hayo wakati akihutubia wakazi wa mji wa Kasese magharibi mwa Uganda baada ya tukio la kuuawa kwa wanafunzi 40 na wengine kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi.
‘’Walikuja hapa wakalala siku mbili, ndio wakaja kuchoma watu, walitaka kuchoma magari ,wakaona magari ya jeshi wakarudi kwenye shule, sasa hivi tumetuma ndege kila sehemu inaenda kuwatafuta, tunataka kuokoa wale waliwateka wakaondoka nao’’
Gen Olum aliongeza kuwa waasi hao walifika katika eneo hilo la magharibi na kukaa kwa siku mbili kabla ya kufanya tukio.
"Tumepata habari kwamba waasi walikaa hapa kwa siku mbili kabla ya kuvamia shule, ndio wakahakikisha wanakuja wanafunga mlango kwa vijana,. vijana walijaribu sana kupigana lakini walihakikisha wamechoma magodoro yao, nguvu ikawashinda, kwa wasichana walikuta mlango wazi, ndio wakaua na kukatakata’’ anasema Gen Olum.
Shambulio dhidi ya shule hiyo ni tukio la kwanza la aina hiyo ndani ya Uganda kwa miaka mingi.
Mnamo 1998, waasi wa ADF walishambulia Taasisi ya Kiufundi ya Kichwamba wilayani Kabarole na kuwachoma moto wanafunzi 80 hadi kufa na kuwateka nyara zaidi ya 100.
Kundi la ADF liliundwa mashariki mwa Uganda katika miaka ya 1990 na kuanza vuguvugu dhidi ya Rais wa muda mrefu, Yoweri Museveni, kwa madai ya mateso ya serikali dhidi ya Waislamu.
Baada ya kushindwa na jeshi la Uganda mwaka 2001, ilihamia jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC.
Mwanzilishi mkuu wa kundi hilo, Jamil Makulu, alikamatwa nchini Tanzania mwaka 2015 na yuko kizuizini katika gereza la Uganda.
Waasi wa ADF wamekuwa wakiendesha shughuli zao kutoka ndani ya DRC kwa miongo miwili iliyopita.