Kundi la waasi la M23 Movement (M23) linatarajiwa kujiondoa kabisa katika maeneo muhimu katika jimbo la Nord Kivu mashariki mwa DR Congo.
Wanajeshi wa Kikosi cha Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) watachukua maeneo ambayo waasi hao walisalimu amri, ambao kuibuka kwao tena mwishoni mwa 2021 kumesababisha vifo vya mamia na maelfu ya wengine kuyahama makazi yao.
Mpatanishi maalum wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uhuru Kenyatta, alisema tarehe 4 Aprili kwamba M23 watajiondoa katika maeneo zaidi ya Nord Kivu kufikia leo.
Hapo awali EAC iliweka makataa ya Machi 30 kama siku ya mwisho ya kujiondoa.
Wakati huo huo, duru ya nne ya mazungumzo yenye lengo la kuleta utulivu eneo la mashariki mwa Congo yanatarajiwa kurejelewa tena hivi karibuni huko Goma, Beni, Uvira, Bukavu na Bunia.
Duru tatu za awali zilifanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.