Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waasi M23 waendeleza mapigano DRC

Waasi Wa M23 Waunga Mkono Harakati Za Kuleta Amani DR Congo Waasi M23 waendeleza mapigano DRC

Sun, 12 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mapigano yameendelea kuripotiwa kati ya jeshi la serikali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC na waasi wa kundi la M23 mashariki mwa nchi hiyo ambapo kwa sasa mapigano hayo yameshika kasi kwenye eneo la Sake jimboni Kivu Kaskazini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York, kwamba mapigano hayo yamesababisha wakazi wengi wa Sake kukimbilia makao makuu ya Kivu kaskazini, Goma, huku wengine wakikimbilia jimbo la Kivu Kusini.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO umetuma kikundi cha doria kwenye eneo kati ya Sake na Goma huku ukiendelea na juhudi za kuwalinda raia.

“Ujumbe huo pia unaendelea kuratibiana na wadau wa utoaji misaada ya kibinadamu ili kutathmini hali ya mahitaji na hatimaye kupunguza machungu kwa raia,” amesema Bwana Dujarric.

Wakati huo huo, ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa umekuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa DRC Jean-Michel Sama Lukonde Kyenge kwenye mji mkuu, Kinshasa.

Mazungumzo baina ya pande hizo hili yamejikita kwenye vipaumbele kama vile upokonyaji silaha na uvunjaji makundi ya waasi nchini humo, miradi ya kukwamua na kuweka utulivu kwenye jamii pamoja na michakato ya Nairobi na Luanda ambayo yote inalenga kupunguza mvutano na kuleta amani mashariki mwa nchi hiyo.

Mchakato wa Nairobi, unaongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambapo hivi karibuni katika mkutano wa wakuu wa nchi uliofanyika nchini Burundi, viongozi hao walitoa taarifa ya pamoja ya kukariri wito wao wa kutaka kusitishwa mapigano huko mashariki mwa DRC.

Na kwa upande wa mchakato wa Luanda, unaongozwa na Rais João Lourenço wa Angola ambaye amewaleta pamoja Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Felix Tchisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na msuluhishi wa mzozo huo kutoka EAC ambaye ni Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta.../

Chanzo: www.tanzaniaweb.live