Zaidi ya watu 1,000 nchini Liberia, wameshiriki maandamano ya kupinga ugumu wa maisha na kitendo cha Rais wao, George Weah kuwa na safari nyingi na kukaa nje ya nchi kwa muda mrefu huku wao wakikosa majibu na hatma ya maisha yao.
Watu hao, kwa mara kadhaa wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ikiwemo mji mkuu wa nchi hiyo, Monrovia na yakifanyika katika uongozi wa miaka mitano wa rais huyo huku wakihoji ni namna gani serikali inavyosimamia uchumi wa nchi.
Hata hivyo, baadhi ya waandamanaji hao wamesema bei za chakula na nishati zimepanda kutokana na athari za janga la Uviko-19 na vita vya nchini Ukraine na kwamba wameandaa ushinikizaji huo kwa maandamano ya amani yaliyofanyika kwa kushirikiana na vyama vikubwa vinne vya upinzani.
Rais wa Liberia, George Weah amekuwa nje ya nchi tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2022 akiitembelea Qatar kumwangalia mwanawe, Timothy Weah, aliyechezea timu ya Marekani katika Kombe la Dunia na pia kuhudhuria mkutano wa Marekani na viongozi wa Afrika mjini Washington huku akitarajiwa kurudi hapo kesho jumatatu Desemba 19, 2022.