Gadi ya Kitaifa ya Ulinzi wa Pwani ya Tunisia imetangaza habari ya kuaga dunia wahamiaji 29 kati ya 34 wa Kiafrika waliotoweka Ijumaa iliyopita baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuelekea Ulaya kuzama baharini karibu na pwani ya Tunisia.
Msemaji wa gadi hiyo, Houssameddine Jebabli amesema wavuvi wa Tunisia wamefanikiwa kuopoa miili 19 kutoka baharini, na kwamba wahajiri hao walikufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka katika pwani ya mji ya Sfax.
Ameongeza kuwa, usiku wa kuamkia jana Jumapili, Gadi ya Kitaifa ya Ulinzi wa Pwani ya Tunisia iliopoa majini maiti 8, na kwamba wahajiri 11 wameokolewa. Aidha amesema maiti nyingine 2 zimegunduliwa katika pwani ya mji ya Sfax.
Asasi moja isiyo ya kiserikali ya Tunisia imesema boti tano zimezama baharini katika pwani ya Sfax katika kipindi cha siku mbili, na kwamba wahajiri 67 waliokuwemo kwenye vyombo hivyo vya usafiri wa majini hawajulikani walipo mpaka sasa.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, wahamiaji wasiopungua 12,000 ambao wamefanikiwa kufika nchini Italia mwaka huu, waliingia kwa boti kupitia Tunisia, ikilinganishwa na watu 1,300 katika kipindi kama hicho mwaka 2022. Hapo awali, Libya ilikuwa sehemu kuu ya kivuko iliyokuwa ikitumiwa na wahamiaji kutoka Afrika.
Ukanda wa pwani wa mji wa Sfax umekuwa mashuhuri ukitumiwa na watu wanaokimbia umaskini na migogoro katika nchi za Afrika na Asia Magharibi na kujaribu kutafuta maisha bora katika nchi za Ulaya.
Mapema mwezi huu wa Machi, mamia ya wahajiri wa Kiafrika walianza kurejea katika nchi zao wakitokea Tunisia, baada ya Rais Kais Saied wa nchi hiyo kutoa matamshi yaliyoonekana kuwa dhidi ya wahamiaji nchini humo.