Shirika la Afya Duniani laonya kuhusu hatari ya kibiolojia nchini Sudan Shirika la Afya Duniani limeonya juu ya hatari za kibaolojia baada ya maabara hatari ya kemikali kuangukia mikononi mwa mmoja wa pande zinazohusika katika mzozo nchini Sudan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Shirika la Afya Ulimwenguni WHO lilitangaza jana Jumanne kwamba kuna hatari kubwa ya kibiolojia mjini Khartoum baada ya mmoja wa pande zinazohusika katika mzozo wa Sudan kuchukua udhibiti wa maabara ya kemikali hatari. Vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu na surua na vitu vingine hatari vimehifadhiwa katika maabara hiyo. Nima Saeed Obeid, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani nchini Sudan, amesema kuwa, wataalamu wa masuala ya kiufundi hawana uwezo wa kuifikia maabara ya afya ya umma kuhakikisha usalama wa vifaa vilivyomo.
Hata hivyo amekataa kusema ni upande gani wa mzozo nchini Sudan unaidhibiti maabara hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Shirika la Afya Ulimwenguni, mapigano ya kijeshi kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Radiamali ya Haraka yaliyoanza Aprili 15 yamesababisha vifo vya watu 459 huku watu elfu na 72 wakijeruhiwa. Lakini mwakilishi wa shirika hili la kimataifa nchini Sudan anaamini kwamba idadi ya waliokufa ni kubwa zaidi kuliko hiyo iliyotangazwa na yeye mwenyewe ameona miili ya watu iliyoizagaa mitaani katika siku za hivi karibuni. Shirika la WHO pia limeripoti kutokea mashambulizi 14 kwenye vituo vya afya tangu ulipoanza mzozo huo. Pande hasimu zimekubaliana kusitisha vita kwa muda wa siku tatu, lakini baadhi ya taarifa zinasema kuwa, makubalilano hayo hayaheshimiwi.