Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa linalofuatilia vifo vya watoto limebaini kuwa watoto wengi waliofariki kabla ya siku zao za kuzaliwa walitoka barani Afrika.
Utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kukadiria Vifo vya Watoto linaonesha kuwa watoto milioni tano walikufa mwaka 2021. Hata hivyo, viwango vya vifo miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara vimekuwa vikipungua tangu mwaka 2000.
Licha ya kuongezeka kwa idadi ya watu barani Afrika ambako kunakuja na changamoto zake, ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa kuongezeka kwa chanjo, uwekezaji katika mifumo muhimu ya afya kwa wanawake wanaojifungua hospitalini ni baadhi tu ya sababu ya kupungua kwa vifo.
Lakini bado kuna kundi la watoto ambao hawapati kusherehekea miaka mitano yao ya kuzaliwa- wale waliozaliwa katika nchi ambazo zina migogoro ya ndani na hali ya usalama si nzuri, ufadhili duni wa serikali ili huduma za afya ya msingi na programu za utapiamlo.
Baadhi ya nchi zilizotajwa ni DR Congo, Mali, Burkina Faso, Nigeria, Chad, Niger, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ripoti hiyo inatoa wito kwa serikali katika nchi hizi kuongeza huduma bora za afya hasa wakati wa kujifungua. Pia wanasema kuwa ukusanyaji wa data ulioboreshwa utasaidia kuja na sera na programu zilizoundwa kwa ajili ya maisha bora ya kikundi hiki cha umri.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonya kwamba ikiwa suluhu hazitawekwa mapema, watoto zaidi wataendelea kufa kutokana na vifo vinavyoweza kuzuilika.