Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limesema kuwa, linahitaji kwa dharura dola milioni 137 za Kimarekani ili kuliwezesha kugawa chakula kwa wakimbizi wapatao milioni 1.5 nchini Uganda katika miezi ijayo.
Abdirahman Meygag, mkurugenzi wa WFP nchini Uganda ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "WFP nchini Uganda hivi sasa ina uhaba mkubwa wa fedha na kuna hatari ya kweli ya kukatika kabisa misaada yake katika miezi ijayo."
Aidha ameandika: "Ili iweze kuendelea kutoa msaada wa chakula wa kuokoa maisha wakimbizi, WFP inahitaji kwa haraka dola milioni 137. Haki ya chakula ni haki ya binadamu."
Matamshi hayo yamekuja siku moja tu baada ya Uganda juzi Jumanne kuungana na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani.
Kwa mujibu wa WFP, Uganda ndiyo nchi inayohifadhi wakimbizi wengi zaidi barani Afrika, ikiwa na takriban wakimbizi milioni 1.5, hasa kutoka nchi jirani kama vile Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Somalia.
Huku hayo yakiripotiwa, Jeshi la Uganda limesema kuwa, limewaokoa wanafunzi watatu na watu wengine watatu katika kampeni ya kijeshi ya kuwasaka wa Allied Democratic Forces (ADF) ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya magaidi hao kufanya shambulio baya dhidi ya skuli moja ya nchi Uganda, wiki iliyopita.
Felix Kulayigye, msemaji wa jeshi la Uganda, amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, watu sita hao wameokolewa kwenye msako unaoendelea wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda la ADF ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika sehemu moja ya matamshi yake, msemaji huyo wa jeshi la Uganda amesema: "Ni kweli katika operesheni na msako mkali unaoendelea kwenye Hifadhi ya Taifa ya Virunga, wanafunzi watatu kati ya sita waliotekwa nyara na magaidi wameokolewa. Aidha, mwanamke mmoja na watoto wawili wameokolewa msituni. Juhudi zote zinafanywa ili kuhakikisha genge hili (ADF) linaangamizwa, na wale watoto waliosalia (wanafunzi) wanaokolewa."
Watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa ADF walishambulia Skuli ya Sekondari ya Lhubirira iliyoko Mpondwe katika wilaya ya Kasese ya magharibi mwa Uganda, takriban kilomita 2 tu kutoka mpaka wa nchi hiyo na DRC. Katika uvamizi wao huo uliofanyika tarehe 16 mwezi huu wa Juni, magaidi hao waliua wanafunzi wasiopungua 37, mlinzi mmoja na watu watatu wa jamii ya eneo hilo.