Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WFP: Watoto milioni 1.6 kukumbwa na utapiamlo Sudan Kusini

Utapiamlo Sudan Sudan.jpeg WFP: Watoto milioni 1.6 kukumbwa na utapiamlo Sudan Kusini

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula la Duniani WFP limeonya kwamba watoto katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko nchini Sudan Kusini wanatarajiwa kukabiliwa na viwango vya juu vya utapiamlo katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024 huku janga la mabadiliko tabianchi likizidi kushika kasi katika taifa hilo la Afrika ya Mashariki.

Taarifa iliyotolewa na WFP Mjini Juba nchini Sudan Kusini imemnukuu Mwakilishi wa WFP nchini humo Mary-Ellen McGroarty akisema “huu ndio uhalisia wa kuishi katika mstari wa mbele wa janga la mabadiliko ya tabianchi.”

Bi. McGroarty akifafanua zaidi ameeleza “Tumeona kuongezeka kwa utapiamlo ambao ni matokeo ya moja kwa moja ya kuishi katika hali ya msongamano na maji mengi, kuenea kwa magonjwa yatokanayo na maji na kuondoa kabisa kazi zozote zilizofanywa na mashirika ya misaada ya Kibinadamu katika kuzuia na kutibu utapiamlo kwa watoto wadogo ambao ndio wanaathiriwa vibaya.”

WFP imeeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti ya uhakika wa kupata chakula IPC, zaidi ya watoto milioni 1.6 walio na umri wa chini ya miaka mitano wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mwaka 2024, huku maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko yakitarajiwa kukabiliwa na utapiamlo mbaya zaidi kutokana na kuenea kwa magonjwa yanayosambazwa na maji na msongamano wa watu.

Ongezeko hilo limeelezwa kuchangiwa zaidi na raia wa Sudan Kusini waliorejea katika taifa hilo wakikimbia mapigano nchini Sudan, kwani watakabiliwa na hali mbaya zaidi ya uhaba wa chakula.

Kaunti ya Rubkano ambayo maji ya mafuriko yamezamisha kabisa jamii nzima au kuziweka kwenye visiwa vidogo tangu mwaka 2021, imetajwa kuwa katika mstari wa mbele kukabiliwa na viwango vya juu na vikali wa utapiamlo kufikia mwezi Aprili 2024.

WFP inakabiliana na vikwazo vikubwa vya uhaba wa ufadhili na mtazamo wa rasilimali kwa mwaka 2024 bado ni mbaya, wakieleza ni theluthi moja tu ya watoto wenye utapiamlo wa wastani wanaohitaji matibabu watafikiwa kufikishiwa huduma kutokana na uhaba wa fedha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live