Mashirika ya habari nchini Burkina Faso yameushutumu utawala wa kijeshi kwa ukandamizaji baada ya Redio ya Kimataifa ya Ufaransa, RFI kutakiwa kusimamisha matangazo yake.
Katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni, wakuu wa vyombo 10 vya habari, wamesema waandishi Habari wanakabiliwa na shinikizo la kila siku kutoka kwa viongozi au makundi yenye ushawishi katika jamii.
Taarifa ya viongozi hao imeeleza kuwa kusema au kuandika ukweli, imekuwa uhalifu ambao vyombo vya habari vinaweza kusimamishwa kuendesha shughuli zake bila kufuata utaratibu.
Desemba 3, utawala wa kijeshi uliamuru RFI kusitisha mara moja matangazo yake kwa muda usiojulikana.
RFI ilishutumiwa kwa kutangaza kilichoelezwa kama "ujumbe wa vitisho" kutoka kwa kiongozi wa kigaidi.
Aidha, taarifa hiyo imesema wanahabari wawili maarufu Lamine Traore na Newton Ahmed Barry wamekuwa wakipokea vitisho vya kuuawa kupitia mitandao ya kijamii.