Watu sita wameuawa baada ya kupigwa risasi katika maandamano ya Azimio la Umoja Kenya yaliyohusisha vurugu kati ya polisi na waandamanaji.
Kati ya waliouawa, watatu walipigwa risasi katika Mji wa Kitengela, mmoja huko Emali na wawili walipigwa eneo la Mlolongo kaunti ya Nairobi.
Takriban watu sita walifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita kufuatia maandamano hayo na sasa idadi ya vifo kufikia 12.
Kwa mujibu wa polisi, zaidi ya watu 10 ni majeruhi.
Mtandao wa Nation, unaeleza kuwa waandamanaji huko Emali walichoma gari la polisi na kurusha mawe kwenye majengo ya benki moja, hali iliyosababisha shughuli za kiuchumi kusimama.
Waandamanaji hao wanaoipinga Serikali, wanadaiwa kujihusisha na uporaji pamoja na kuharibu miundombinu pembezoni mwa barabara eneo la Mlolongo, jijini Nairobi.
Pia, madereva wa usafiri wa umma katika sehemu tofauti za nchi waligoma wakidai bei ya mafuta ipo juu.
Kaunti zilizoshiriki maandamano hayo na barabara kufungwa ni Kisii, Nyamira, Migori, Kisumu, Nairobi, Nakuru, Machakos, Murang’a, Mombasa na Kilifi.
Mgomo wa Daladala
Wananchi katika baadhi ya maeneo walilazimika kutembea ili kufika maeneo yao ya kazi.
Mjini Nyeri, vituo vitatu vya mabasi vilibaki bila watu baada ya wafanyakazi kuitikia wito wa mgomo huo.
Madereva waliokuwa wamegoma walifanya msako kuwatafuta waliokuwa wakiendelea na shughuli zao na kuwafukuza.
Dereva wa daladala mjini Nyeri, Onesmus Githinji alisema hawataruhusu baadhi ya wenzao kuendelea na kazi huku wao wakiwa kwenye mgomo.
“Bei ya mafuta inatuathiri wote. Ikiwa kuna mgomo, wote tugome. Hakuna anayepaswa kuendelea na kazi,” alisema Githinji.
Hata hivyo, wananchi katika mji huo ambao ni ngome ya makamu wa Rais wa Kenya, Rigath Gachagua, walijiunga na maandamano hayo ya kupinga gharama za juu za maisha.
Kuahirishwa mkutano
Kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga alilazimika kuahirisha mkutano wake uliopangwa kufanyika katika viwanja vya Kamukunji jijini Nairobi, akisema wamepokea taarifa za watu maalumu kuamrishwa kuwapiga risasi waandamanaji watakaokusanyika eneo hilo.
Odinga alisema baadhi ya wafanyakazi wao waliokuwa wakifanya maandalizi katika viwanja hivyo walishambuliwa na polisi.
“Jana usiku (juzi) tulipokea taarifa za mpango mbaya wa Kenya Kwanza kutuma majambazi kuwavamia waandamanaji wetu katika mkutano wa Kamukunji. Majambazi hawa wamepewa amri ya kufyatua risasi moja kwa moja kwa watu wetu,” alisema Odinga.
Hata hivyo, polisi walifanikiwa kuwatawanya waandamanaji waliofika katika viwanja hivyo kwa ajili ya mkutano wa upinzani.
Mabomu ya machozi yaathiri wanafunzi
Zaidi ya wanafunzi 50 walikimbizwa hospitali baada ya maofisa wa polisi kulipua mabomu ya machozi karibu na shule moja huko Kangemi jijini Nairobi.
Moshi wa mabomu hayo uliwaathiri wanafunzi waliokuwa darasani.
Kwa mujibu wa mmoja wa wenyeji wa eneo hilo, bomu la machozi lilirushwa darasani na maofisa wa polisi waliokuwa wakiwatawanya wakazi waliojitokeza katika maandamano ya Azimio.
“Ndiyo, kulikuwa na wanafunzi zaidi ya 50. Tumefanikiwa kudhibiti hali hiyo, wengi wao sasa hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Dk Aron Shikuku.
Odinga asema ujumbe umefika
Akizungumza katika ukumbi wa Jaramogi Oginga Odinga baada ya kuahirisha mkutano, Odinga alisema Wakenya wamechoka na ujumbe wao sasa umefika kwenye mamlaka, huku akiongeza kwamba wamechoshwa na ahadi za uwongo.
“Watu wamejitokeza hata katika maeneo ya ndanindani nchini. Ujumbe umeeleweka na ni wazi kwamba Wakenya wamechoka,” Raila alisema.
Alisema kujitokeza kwa waandamanaji nchi nzima kunamaanisha wananchi wamedhamiria kujiamulia jinsi watakavyoendesha maisha yao.
“Watu wamechoshwa na sheria kandamizi na askari kila mahali ambao malengo yao ni kuchukua kila sarafu tunayozalisha na kuipeleka kwa Ruto kama ushuru, huku sisi tukibaki bila chochote kwa ajili ya familia zetu,” alisema Odinga.
Juzi, wakati Rais William Ruto akizungumza na wananchi nchini humo alisema hataruhusu maandamano kuendelea nchini humo kwani muda uliopo ni wakati wa kufanya kazi.
“Uchaguzi ulishaisha, wakitaka madaraka wasubiri kipindi kingine cha uchaguzi. Siwezi kuruhusu maandamano kuendelea hapa nchini, siwezi kuruhusu maisha ya Wakenya kupotea,” alisema Rais Ruto.