Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita ya Kenyatta, Ruto yashika kasi

KENYATTA NA RUTTO Vita ya Kenyatta, Ruto yashika kasi

Mon, 6 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Washirika wa Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta wamemshutumu mrithi wake, Rais William Ruto, kwa kile walichokiita kuvuka mipaka, huku wakizungumza kwa ghadhabu kuhusu hatua ya Serikali ya kumpunguzia walinzi Kenyatta.

Maoni ya wanasiasa wa Muungano wa Azimio la Umoja yalikuja juu huku Inspekta Jenerali wa Polisi, Japhet Koome akithibitisha jana kuwa amewaita maofisa wa vyeo vya juu katika kikosi cha ulinzi wa mkuu huyo wa nchi wa zamani.

Koome alieleza kwamba kuwaondoa maofisa hao ni utaratibu wa kawaida wa kujipanga kwa maofisa usalama wa Rais wa zamani.

“Hiki ni kisasi binafsi. Ikulu inapaswa kuwa ofisi inayowaleta watu pamoja sio kuwagawanya. Unatuambia kwamba tuko kwenye wakati mgumu. Kama upinzani, tunasema hapana. Kuondolewa kwa walinzi ni kosa,” alisema aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa, Jeremiah Kioni.

“Hii ni kisasi binafsi wakati Wakenya wanajiuliza ni nani atawaokoa kutoka kwenye matatizo mengi yanayowakabili sasa. Unamtendeaje vibaya mtu ambaye anaongoza mipango ya amani katika nchi nyingine?” aliongeza.

Ilibainika kuwa maofisa 96 wa cheo cha juu wanaohusishwa na Kenyatta walipunguzwa hadi kufikia 25, huku mke wa Rais wa zamani akisaliwa na walinzi watano.

IGP Koome jana alisema kama ofisa katika cheo cha mkaguzi mkuu msaidizi, mkuu wa kikosi cha ulinzi wa Rais wa zamani alikuwa na cheo kikubwa mno na ilitakiwa awe wa cheo cha chini.

Kuondolewa kwa walinzi wa Rais huyo wa zamani, kumekuja wakati washirika wa Rais Ruto wakiishutumu familia ya Kenyatta kwa kukwepa kodi na kuwa nyuma ya mikutano ya kisiasa ya chama cha upinzani. Kenyatta, wiki iliyopita aliushutumu utawala wa Ruto kwa kuwapa Wakenya ahadi tupu.

Ilimtokea Ruto pia

Kilichotokea kwa Kenyatta, kilitokea kwa Rais Ruto Agosti 2021 wakati akiwa Naibu wa Rais, ambapo walinzi wake waliondolewa katika makazi yake rasmi yaliyopo Karen, Nairobi.

Maofisa usalama kutoka kampuni ya GSU G ambao walikuwa wakilinda makazi hayo, waliondolewa na nafasi zao kuchukuliwa na Jeshi la Polisi wa Kitengo cha Majengo ya Serikali (AP SGB).

Hata hivyo, taarifa kutoka ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi ilisema kubadilishwa kwa walinzi hao lilikuwa ni jambo la kawaida.

“Huu ni upangaji upya wa majukumu katika huduma ya kitaifa ya polisi ili kuongeza ufanisi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Akiwa kwenye msiba wa aliyekuwa Waziri wa Elimu wakati wa utawala wake, Kenyatta aliukosoa utawala wa Rais Ruto kwamba umekuwa ukitoa ahadi hewa kwa wananchi, lakini wameshindwa kutekeleza yale waliyowaahidi kwenye kampeni za uchaguzi wa Agosti 2022.

“Kuna watu wa aina mbili. Kuna watu wanaongea sana kuhusu watakachofanya lakini hawafanyi chochote na hao ni wengi. Lakini kuna watu watazungumza kidogo na matendo yao yataonekana,” alisema Kenyatta.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live