MUUNGANO wa makanisa nchini Uganda unataka Katiba ifanyiwe marekebisho na kusitisha uchaguzi wa Januari 14 ili kumruhusu Rais Yoweri Museveni kuendelea kuwa madarakani kwa muda wa miaka mitatu zaidi.
Muungano huo umesema mazingira ya sasa nchini humo hayaruhusu kufanyika uchaguzi huru na wa haki. Viongozi hao wa dini wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Uganda, Dk Cyprian Kizito Lwanga wamesema Katiba inatakiwa kufanyiwa marekebisho na uchaguzi kuahirishwa kutokana na janga la virusi vya corona.
Walisema wamefikia hatua hiyo baada ya majadiliano ya muda mrefu yaliyoangazaia janga la virusi vya corona na hali ya kisiasa ilivyo hivi sasa nchini ambayo wameeleza hayaruhusu kufanikisha uchaguzi ulio huru na haki.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Kampala juzi, Dk Lwanga alisema Bunge linatakiwa kuchukua hatua za haraka na kufanyia marekebisho Katiba ili kuongeza muda wa utawala wa sasa kwa miaka mitatu zaidi.
Kwa mujibu wa viongozi hao wa makanisa, wanasiasa wanapuuza kanuni za maofisa wa afya juu ya namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona hivyo kuwapo ongezeko la maambukizi na vifo vingi vya wananchi.
Aidha, wamewakosoa maofisa wa usalama kwa kuwakandamiza wagombea wa upinzani, kuwakamata, kuwazuia kufanya kampeni, kutumia gesi ya kutoa machozi kutawanya mikutano ya kampeni na kuwapiga wafuasi wa upinzani.
Kwa mujibu wa Katiba ya Uganda, uchaguzi unapoahirishwa, Spika wa Bunge anapaswa kuongoza serikali. Zimebakia karibu wiki tatu kufanyika kwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Januari 14 mwakani.